HIVI, UNAZIFAHAMU NJIA AMBAZO UNAWEZA KUZITUMIA KUPATA KAZI HARAKA?

0

“Sisi tunatamani fursa, tunaomba kwa ajili ya fursa na tunahangaika kutafuta fursa. Habari njema ni kwamba kila wakati tunakutana na fursa. Habari mbaya ni kwamba ni sisi wenyewe tunazipoteza fursa, na kuja kutambua baadaye kwamba tumepoteza fursa”
Mwisho wa kunukuu maneno ya- Ernest Agyemang Yeboah, ambayo tunaweza kuyatumia katika Makala hii kuwakumbusha wahitimu wanaotafuta kazi kuwa fursa inapotokea sharti itumiwe.

Kila mwaka maelfu ya wanafunzi wanahitimu masomo yao ya elimu ya juu na kuingia katika mchakato wa kutafuta ajira. Idadi ya wanafunzi wanaomaliza, ukiilinganisha nafasi za ajira huwa haviendani kabisa na unaweza ukajiuliza; je, ni wangapi watafanikiwa kuajiriwa?

Jibu haliwezi kuwa rahisi, ila kila mmoja wetu anatambua kuwa miongoni mwa wahitimu hao wanatofautiana jitihada na mbinu za kutafuta kazi. Naweza kusema kuwa atakayewahi kupata ni yule wakwanza kuitafuta fursa.Iwe kwa kuunganishiwa na mtu anayemfahamu au juhudi zake binafsi za kwenda mlango hadi mlango wa ofisi mbali mbali kuomba ajira.

Kipindi cha kumaliza masomo na kutafuta ajira kwa wahitimu huwa ni kipindi cha vita kali ya ushindani wa vigezo baina yao. Ushindani unakuwa mkubwa, kiasi kwamba kwa kila kazi moja inayotangazwa kuna waombaji zaidi ya elfu moja wanaigombania.,wengine wakiwa na sifa, na wengine ambao wamekosa sifa za kupata hiyo kazi, lakini wote wanakuwa na nafasi sawa. Kujua tu, wapi kuna nafasi za kazi ni juhudi binafsi ya mhitimu mwenyewe kufanya mbinu zake.

Hebu leo tuangalie mbinu ambazo unaweza kuzitumia ili kupata ajira kwa haraka:

TENGENEZA MTANDAO NA WAHITIMU WENZAKO
Kubali usikubali miongoni mwa wahitimu, wengine wanawahi sana kupata kazi. Hawa ndio mara nyingi wanaitwa walio kwenye mfumo, na wengi wetu tunaonaga wanapendelewa kwa kuwa wanajuana na watu katika soko la jira. Mtu kama ukishamfahamu jaribu kujenga ukaribu nae, mng’ang’anie usimuache,kwani wao mara nyingi wanauwezo wa kufahamu au kuambiwa kwa haraka mahali ambapo ajira zimetangazwa. Wao ndio watakuwa wakwanza kukujulisha kama kuna sehemu kuna nafasi za kazi zimetangazwa.

SOMA MATANGAZO MBALIMBALI YA KAZI
Ukiwa unajizoesha kusoma matangazo mbali mbali ya nafasi za kazi utaweza kujua sifa gani
hasa zinahitajika. Ukiweza kufanya hili maana yake hautakurupuka kuandika wasifu wako, na kutuma haraka haraka kwa kuwa tu umeliona tangazo. Ukiwa makini kuandaa wasifu, ambao umeweka sifa ambazo mwajiri ndio anazihitaji utaongeza nafasi yako ya kuitwa katika usaili na kupata kazi kwa haraka. Hapa kwetu njia kubwa inayotumika ni magazeti, na siku hizi kuna mitandao ya ajira, ukienda sehemu kama maktaba ya taifa utakutana na magazeti hadi ya miaka mitano nyuma, hebu fuatilia sifa za waajiliwa zinazohitajika, zinavyobadilika mwaka hadi mwaka ili ujiandae.

SOMA SANA TAARIFA YA KAMPUNI ULIZOOMBA KAZI WAKATI UNASUBIRI USAILI
Wakati unasubiri, kama utaitwa katika usaili au la, usikae vijiweni kupiga stori tu, kila siku fuatilia taarifa za kampuni uliyoomba kazi hata kama ni kumi fuatilia zote kwani hujui ipi itakayoanza kukuita. Hii itakusaidia kutambua malengo ya kampuni hiyo na wapi inataka kuelekea na kama wana mpango wa kuongeza au kubadilisha aina ya huduma au bidhaa wanayotoa kwa jamii. Unapokuwa na taarifa za kutosha kuhusu kampuni uliyoomba kazi itakupa ujasiri wa kuzungumza na kutoa majibu kuhusu kampuni hiyo wakati wa usaili.

UWE TAYARI KUJITETEA
Yawezekana kabisa, ukawa umetuma maombi yako ambayo yamepishana kidogo sana na hitaji la mwajiri lakini yanaendana kinamna fualni, jiandae na utetezi wakati wa usaili, kwa kuwadhirishia kuwa mpishano huo mdogo hautakuzuia wewe kujifunza kitu kipya Sio kusema tu kuwa unaweza kazi waonyeshe unajua na unaweza kufanya kazi nzuri.

KUWA TAYARI KUJITOLEA
Wakati unasubiria kupata kazi ya kudumu usijilemaze, kukaa bila kitu cha kufanya mitaani. Nenda katika kampuni ndogo, ambazo zinashughulika na masuala uliyosomea na jitolee kufanya kazi bure bila malipo. Hii itakupa uzoefu na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuajiliwa hata hapo hapo.

HUDHURIA MAONYESHO YA MAKAMPUNI
Katika nchi yoyote, makampuni mengi huwa yana utaratibu wa kufanya maonyesho wa shughuli zao. Ukiwa na utaratibu wa kuhudhuria matukio kama haya, yatakusaidia kuwafahamu baadhi ya wafanyakazi na kuwadadisi kwa undani kazi zao za kila siku hasa kile kitengo ulichosomea wewe.Mathalani umesomea uhasibu unaweza kumuuliza mfanyakazi huyo majukumu ya mhasibu katika kampuni hiyo na ugumu anaoupata.

JITENGENEZEE KADI ZA MAWASILIANO
Utaratibu wa kubadilishana mawasiliano, baina ya mtu na mtu ni mzuri pale unapotumiwa vizuri. Utaratibu huu utamfanya uliyekutana naye akuone jinsi gani uko makini, sio mpaka uwe na biashara au kampuni ndio utengeneze kadi ya mawasialiano yako.

NENDA MWENYEWE SEHEMU HUSIKA
Ukitegemea sana watu wengine ndio wakutafutie kazi wewe, utakuwa unapoteza bahati yako ya kuajiriwa mapema. Yawezekana kabisa, kampuni inajiandaa kutoa tangazo la kazi kesho wewe umepeleka leo,na una vigezo kwanini wasikuchukue kuliko kuandaa gharama za matangazo.Si utakuwa umefanikiwa hapo!

ENDELEZA UNADHIFU
Najua wahitimu wengi tunanawiri na kupendeza pale tulipokuwa mazingira ya masomo,lakini tunapoingia mtaani tunajiacha hovyo. Na jua wazi muonekano wako una alama zake kwa mwajiri,kama uko hovyo hovyo hata yeye kukuajiri atajiuliza mara mbili mbili.
Unapotaka kuajiriwa lazima utambue kuwa mwajiriwa yeyote ni mwakilishi wa ile kampni anayoifanyia kazi, sasa mwonekano wake pia unatoa picha ya utamaduni wa ndani wa ofisi hiyo kwa wateja.Ukiwa na utaratibu wa kuwa nadhifu kila wakati itakusaidia uonekane utakuwa mwakilishi mzuri wa taswira ya ofisi husika.

JENGA MAWASILIANO NA KAMPUNI
Usikate, mawasiliano na kampuni uliyowahi kuomba kazi,hata kama uliitwa katika usaili ila hukubahatika kupewa ajira,watumie ujumbe wa barua pepe kuwa wasisite kukuita ikiwa itatokea nafasi. Na kama wana mtandao ambao unaweza kuhifadhi wasifu wako weka huko halafu subiria maana linapotokea hitaji la mfanyakazi hatua ya kwanza wataangalia katika hifadhi yao kuwa waombaji wangapi na kama wana sifa wanazohitaji. Sasa kama na wewe ulshaweka huko unaweza ukaitwa moja kwa moja.

kila mmoja wetu anajua jinsi gani ajira ni ngumu kupata kwa haraka.lakini taarifa za uongo kuhusu soko la ajira zimejaa nyingi mitaani.usimsikilize mtu mwengine, kuwa ajira hakuna. tumia njia hizo hapo uone wewe mwenyewe kuliko kukatishwa tamaa na mtu mwengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here