Hivi ndivyo viti maalum vinavyopatikana

0

NA MWANDISHI WETU

UMEKUWEPO mzozo baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliofanyika Oktoba 28 hasa baada ya vyama vya upinzani kushindwa vibaya kwenye majimbo.

Mzozo huo unatokana na nafasi ya vyama hivyo kwenye uwakilishi wa viti maalum bungeni, ambapo kila mmoja anazungumza anachojua yeye kwa sababu mbalimbali ikiwemo za kisiasa.

Ipo hivi, Ubunge Viti maalum hutegemea idadi ya kura zote za wabunge na si idadi ya wabunge walioshinda. Kila chama kinachopata walau asilimia tano ya kura zote za wabunge kinapewa viti kadhaa kulingana na jumla ya kura zote za wabunge.

Mfano, mwaka 2015 jumla ya kura zote za wabunge katika uchaguzi zilikuwa 14,574,957. Vyama vilivyofikisha walau asilimia tano ya kura hizi ni CCM (asilimia 55.04), CHADEMA (31.75) na CUF (8.63).

Chama cha ACT-Wazalendo kilikuwa na asilimia 2.22 na NCCR- Mageuzi kiliambulia asilimia  1.50 licha ya kupata mbunge mmoja mmoja bado havikuweza kufikisha walau asilimia tano ya kura zote za wabunge; hivyo kutotimiza vigezo kupata viti maalum.

Aidha, jumla ya viti maalum katika uchaguzi wa mwaka 2015 vilikuwa 110. CCM iliyopata kura zote za wabunge  8,021,427 sawa na asilimia 55.04 ya kura zote, kilipata viti 64. CHADEMA ilipata jumla ya kura zote za wabunge 4,627,923 sawa na asilimia 31.75 ya kura zote za wabunge kilipata viti 36.

Vilevile, CUF ilipata jumla ya kura zote za wabunge 1,257,765 sawa na asilimia 8.63 ya kura zote za wabunge kilipata Viti 10, mgawanyo ulikuwa viti (64+36+10 =110).

Hivyo, kwa hesabu ya mwaka huu kwa upande wa upinzani hali kidogo haijakaa vizuri hasa baada ya kuambulia wabunge wanane kati ya wabunge 264, maana yake hata mgawanyo wao utategemea idadi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here