HISTORIA YA TANGANYIKA KABLA YA UHURU

0

NA JONAS MUSHI

LEO ni siku ya maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru wa Tanzania bara ambayo zamani ilijulikana kama Tanganyika kabla ya kuungana na visiwa vya Zanzibar na kuwa Tanzania.

Kulingana na uzito wa siku hii ambayo itasalia kuwa ya kihistoria kwa Watanzania, naamini kuwa kuna kila sababu ya kuhakikisha  tunatoa darasa kwa kizazi cha sasa ambacho kimekuwa hakina uelewa  mpana juu ya historia hii ya Tanzania bara hasa kabla ya Uhuru.

Hii inachangizwa hasa na kuwapo kwa mabadiliko mbalimbali ya sayansi na hata teknolojia ambayo kwa namna moja ama nyingine yamekuwa yakipelekea kisasi cha sasa kushindwa kutambua na kufuatilia historia ya taifa lao.

Hivyo basi kama ndivyo ungana na mimi kwenye makala hii ambayo naamini kuwa itakuongezea kitu kwenye ufahamu wako wa masuala mbalimbali kuhusu Tanzania Bara mpaka kufikia kupata uhuru wake Desemba 9, 1961.

Kwanza kabisa, Tanganyika kama inavyofahamika ni jina la kihistoria la sehemu kubwa ya Tanzania ya leo, yaani ile yote isiyo chini ya serikali ya Zanzibar kwa maana ya Tanzania Bara.

Kwa sababu za kisiasa, mara nyingi huitwa “Tanzania bara” ingawa ina visiwa pia, hasa Mafia na Kilwa.

Tanganyika ilikuwa eneo lindwa la Uingereza kuanzia 1919 na nchi huru kati ya 1961 hadi 1964, mwaka wa kwanza kama ufalme, halafu kama Jamhuri.

Maeneo yaliyoitwa baadaye (1920) “Tanganyika” yaliunganishwa mara ya kwanza tangu mwaka 1886 kama koloni la Ujerumani lililoitwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Kabla ya kufika kwa ukoloni kulikuwa na madola madogo mbalimbali na maeneo madogo ya kikabila.

Kanda la pwani pamoja na njia za misafara kuelekea Ziwa Tanganyika vilikuwa chini ya athira ya Usultani wa Zanzibar.

Historia inaeleza kuwa tangu mwaka 1885 Karl Peters, kwa niaba ya Shirika la Ukoloni wa Kijerumani (Gesellschaft für Deutsche Kolonisation) alianza kufanya mikataba na watawala wenyeji katika maeneo ya Usagara, Nguru, Useguha na Ukami iliyoweka msingi wa madai yake ya kuchukua utawala mkuu wa maeneo hayo.

 

Uenezeaji wa Wajerumani uliendelea hasa baada ya kushinda upinzani katika vita ya Abushiri na vita dhidi ya Wahehe.

Koloni lile la Kijerumani lilikuwa kubwa kuliko Tanganyika ya baadaye, maana ilijumlisha pia maeneo ya Rwanda na Burundi pamoja na sehemu ndogo ya Msumbiji.

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 – 1918) koloni hilo la Kijerumani lilitekwa na majeshi ya Uingereza na Ubelgiji.

Tunaelezwa kuwa mkataba wa Versailles wa mwaka 1919 ulikuwa na kanuni za kuchukua makoloni yote ya Ujerumani na kuzikabidhi kwa mataifa washindi wa vita. Sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani iliwekwa chini ya utawala wa Uingereza, kasoro maeneo ya Rwanda na Burundi yaliyokabidhiwa mikononi mwa Ubelgiji.

Mwaka 1919 sehemu kubwa ya koloni la Kijerumani ilikabidhiwa rasmi mikononi mwa Uingereza kama eneo la kudhaminiwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa kulingana na kifungo 22 cha mkataba wa Versailles.

Mwaka 1922 Shirikisho la Mataifa lilithibitisha hatua hiyo na kuamua masharti ya kukabidhi, waingereza walihitaji jina jipya kwa ajili ya koloni hilo na tangu Januari 1920 wakaamua kuliita “Tanganyika Territory” kwa kutumia jina la ziwa kubwa upande wa mashariki ya eneo.

Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9, 1961 Historia ya Tanzania, Mwaka 1964 imeunganika na Zanzibar kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here