Historia fupi ya Prof. Manya, naibu waziri wa madini mpya

0

Na Mwandishi Wetu 

Rais Dk. John Magufuli amemteua Profesa Shukrani Manya kuwa mbunge na kisha naibu waziri wa madini ikiwa ni siku mbili baada ya kutengua uteuzi wa Francis Ndulane baada ya kushindwa kusoma kiapo kwa ufasaha.

Ndulane ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini alikuwa miongoni mwa mawaziri 21 na naibu mawaziri 23 walioapishwa mjini Dodoma juzi lakini ilipofikia zamu yake, alihangaika kusoma kiapo kabla ya kutakiwa akapumzike na baadaye rais Magufuli alitengua uteuzi wake na kubainisha kuwa atamteua mtu mwingine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma leo Desemba 11, 2020 na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli amemteua Profesa Manya kuwa mbunge na kisha kuwa naibu Waziri wa Madini na ataapishwa leo mchana Ikulu mjini Dodoma.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Manya amekuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini(TMC) tangu mwaka 2018 baada ya kuanzishwa tume hiyo kupitia Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017.

Kabla ya kuwa mtendaji mkuu, Profesa Manya alianza kukaimu nafasi hiyo kati ya Januari hadi Mei mwaka 2018 wakati huo akiwa kamishina wa madini.

Kabla ya kuanza kuitumikia tume hiyo, Profesa Manya alikuwa mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hadi Desemba mwaka 2017.

Ni mbobezi wa masuala ya Jiolojia aliyesoma UDSM kwa shahada ya kwanza(1994/95), shahada ya uzamili(1999/2001) na uzamivu (2001/2005) huku akianza kufundisha kwa ngazi ya mhadhiri msaidizi mwaka 2001.

Kwa mujibu wa wasifu wake, Profesa Manya ameandika na kushirikishwa katika maandiko ya vitabu mbalimbali vinavyohusisha utafiti wa masuala ya miamba na madini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here