HESLB yataja 47,305 watakaopata mikopo awamu ya kwanza

0
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru

Na Mwandishi Wetu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza orodha ya wanafunzi 47,305 watakaopata mikopo ya awamu ya kwanza.

Imeeleza inatarajia kutumia  Sh Bilioni 150.03 kutoa mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo 2020/2021.

Orodha hiyo imetajwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB,  Abdul-Razaq Badru takribani wiki moja kabla ya vyuo kufunguliwa.

Alisema kati ya wanafunzi 47,305,  wanaume ni 26,964 sawa na asilimia 57.37 na wanawake 20,341 sawa na asilimia 42.63.

“Lengo la mwaka huu ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 54,000 na kwamba kiasi kidogo kilichobaki kitatangazwa siku tajno zijazo,” alisema na kusisitiza:

“Idadi ya wanawake waliopata mkopo mwaka huu imezidi kuongezeka kutoka asiimia 37 mwaka jana na sasa ni asilimia 42.”

Aidha, Badru alisema tayari fedha zimeanza kupelekwa katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu SIPA na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” alisema Badru.

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya awamu ya pili, Badru alisema imepangwa kutolewa Novemba 14, 2020 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji wa mikopo kutembelea akaunti zao za SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

Alibainisha, ambao hawajapangia mkopo kuna taratibu ya kukata rufaa hivyo watapata fursa nyingine ya kutuma maombi yaweze kufanyiwa kazi.

“Tunawakumbusha wanafunzi wote kuendelea kujisali wakifikia vyuoni kwao na wakati wa wiki ya orientention watapewa maelekezo zaidi,” alisema Badru.

Alisema, kwa mara ya pili watatumia mfumo wa kidigitali kufanya malipo hali inayosaidia wanafunzi kupata fedha zao kwa haraka zaidi, ambapo wanafunzi wataingiziwa fedha zao kwenye akaunti ambazo walifungua wakati wanaomba mkopo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here