Hakuna udini Tanzania – Mufti Zubeir

0

Na Hafidh Kido, Korogwe

MUFTI wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Aboubakar Zubeir amewaeleza Watanzania kuwa hakuna udini nchini bali kila mmoja anaheshimu mipaka ya imani ya mwenzake.

Alisema hayo jana katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Korogwe (TTC) wakati wa mkutano wa kampeni za urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

Katika maelezo yake, Mufti Zubeir alisema amani ya nchi ndicho kitu muhimu kinachotakiwa kuzingatiwa kwa sababu bila amani hakuna maendeleo.

“Kabla sijafanya dua kwa ridhaa yako naomba nitoe kitu kilochokuwa kimenikaa rohoni, wananchi lazima waelewe kuwa hakuna udini katika Uislamu. Nimesikia sikia baadhi ya wanaojiita viongozi wa dini wanazungumzia ubaguzi katika dini nasema kwa anayeifahamu vema dini ya kiislamu atajua ukweli.

“Hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu katika Quran aya ya 285 inayozungumzia hakuna kutengana katika dini,” alisema Mufti Zubeir.

Wakati huo huo Mufti alimuomba mgombea urais ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kuna changamoto ya barabara kutoka Korogwe – Mashewa – Daluni hadi Mabokweni anaomba ijengwe kwa kiwango cha lami kwani ni kero kwa wakazi wa maeneo hayo.

Aidha, Dk. Magufuli alionyesha kuguswa na kauli ya
Mufti na kuwakumbusha wananchi waache kuwachagua wagombea wanaotaka kuwagawa kidini, kikabila na kikanda kwa sababu uchaguzi ni kitu cha kupita.

“Mmemsikia Mufti Zubeir hapa aliposema kuhusu amani, amezungumza vizuri sana. Hivyo wale wanaohubiri kujitenga kwa dini kabila na majimbo tuwkatae tusiwape kura,” alisema Dk. Magufuli.

Itakumbukwa hivi karibuni mmoja wa masheikh wanaharakati Ponda Issa Ponda alisimama mbele ya wananchi wakati akimnadi mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu na kudai waislamu wamekubaliana watampigia kura kwa kuwa ndiyo chaguo lao.

Hata hivyo, siku iliyofuata waumini wa dini ya kiislamu walipinga kuwa na makubaliano yoyote katika kipindi hiki cha uchaguzi wala hawana mgombea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here