HAI TUNA JAMBO LETU OKTOBA 28

0
Mgombea Urais kupitiaCCM, Rais Dk. John Magufuli akizungumza na Wananchi wa Hai mkoani Kilimanjaro katika mkutano wa Kampeni za CCM uliofanyika Bomang’ombe Jana Otoba 22, 2020.

NA HAFIDH KIDO, HAI

WANANCHI katika Jimbo la Hai lililopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamekubaliana wana jambo lao ifikapo Oktoba 28 mwaka huu siku ya kupigia kura wagombea urais, ubunge na udiwani, ambapo wamepanga kuwandoa viongozi wa upinzani katika wilaya hiyo.

Wakizungumza na Jamvi la Habari kwa nyakati tofauti kabla ya kumsikiliza mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika Kata ya Bomang’ombe jana walisema mateso waliyoyapata kwa kuzorota maendeleo hawataki kuendelea nayo.

Mzee Suleiman Josaya alisema, katika kipindi chote alichokaa madarakani mbunge wa jimbo hilo Freeman Mbowe hakushuhudia chochote cha kimaendeleo kutokana na mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupendelea siasa za kiharakati badala ya kujali maendeleo.

“Hatukuwa na utulivu, wala hatukuwa na muda ambao mbunge angeweza kuja kukaa na wananchi wake kujadili changamoto zinazotukabili. Kwa kuwa ofisi ya mbunge ipo tunafahamu ameshapelekewa kero zetu nyingi lakini kwa mtindo wake wa maisha hakuweza kuzitatua kwa sababu maisha yake yote ni kupinga hata visivyopingika,” alisema Mzee Josaya na kusisitiza:

“Vijana wameshasema mengi, tunalo la kufanya katika siku ya kupiga kura ili kuondokana nab ala hili tulilonalo. Mambo haya lazima yafikie mwisho.”

Naye Manka John alisema: “Tuna jambo letu tarehe 28 (Siku ya kupiga kura), tumeshakubaliana kwa hiyo hapa kilichopo tunasubiri siku ifike tunaona kama tunacheleweshwa. Ingekuwa ni amri yangu ningemuomba Mheshimiwa Rais (Mgombea urais kwa tiketi ya CCM) akatulie tu Dodoma maana ushindi umeshapatikana.

“Tumeshatubu, tumechoka kutokana na mateso tuliyoyapta tulikuwa tumesuswa. Ndiyo maana unaona njiani kote wananchi wamebeba Masare (Majani ya kimila ya Kichaga yanayoashiria kuomba msamaha). Tunamuomba msamaha Rais Magufuli na chama chake kwa kuwakosea kuwanyima kura za ubunge na udiwani mwaka 2015.”

Akizungumza na wananchi waliomsubiri tangu asubuhi katika viwanja vya Half London, Dk. Magufuli alivutiwa na mwitikio mkubwa wa wananchi tangu njiani wakati akitokea Moshi Mjini, ambapo aliwaambiwa ana deni kubwa la kulipia wema alioonyeshwa na wananchi wa Hai na viunga vyake.

“Nimefurahia mapokez ya heshima mliyonipa huku mmeshikilia masare, nimeelezwa kwa mila za Kichaga majani haya yanamaanisha kuomba msamaha kwa anayeyashika, nataka kuwaambia ndugu zangu hamkunikosea mimi bali mlizikosea nafsi zenu.

“Ndiyo maana nasema wazi kuwa nawapenda, kwa kudhihirisha hilo niliwafanyia mambo makubwa ya kimaendeleo mbali ya kuwa mbunge wenu hakuwa na ushirikiano mzuri na mawaziri, hilo lilinipa wakati mgumu sana,” alisema Dk. Magufuli.

Alibainisha, anakumbuka akiwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alifika katika wilaya hiyo wakati akifuatilia ujenzi wa barabara ambapo alifika katika soko la Sadala akakuta wafanyabishara wadogo wa ndizi na matunda wanasumbuliwa kwa tozo za kero.

Hata hivyo, Dk. Magufuli alibainisha huenda bado kero hizo zinawakabili wananchi wanaofanya biashara katika soko hilo kwa kuwa mbunge wao hakuwa na ushirikiano mzuri na mawaziri ili kutatua kero zinazowakabili wananchi wake.

Alisema, Wilaya ya Hai kwa kukosa baraza imara la madiwani kulimpa wakati mgumu sana ilikuwa ni sawa nakufungwa miguu na mikono kisha wananchi wamuagize awaletee maji, asingeweza kutembea wala kunyoosha mikono kwa kuwa imefungwa kwa kamba.

“Mbunge wenu alipata bahati kwa mujibu wa sheria imara za nchi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipewa uongozi wa kambi ya upinzani bungeni ambapo kwa fedha za walipa kadi alipewa gari la kutembelea, lakini hakuna cha maana alichowafanyia wananchi wake kwa kuwa alikosa ukaribu na mawaziri wangu ambao angewaomba maendeleo,”alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Kazi ya mbunge ni kutafuta mawasiliano na mawaziri, lakini hakufanya hivyo na hata kipindi cha kupitisha bajeti walitoka bungeni wanashindwa kupitisha fedha za kupeleka maendeleo kwenye majimbo yao ndiyo maana jimbo hili la Hai ni miongoni mwa majimbo yenye changamoto nyingi.”

Hata hivyo, alisema mbali ya changamoto hizo lakini bado aliamua kuisaidia Wikaya ya Hai lakini alikutana na changamoto nyingi kwa kuwa alilisaidia jimbo ambalo hakujua wananchi wanataka nini.

Miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali katika miaka mitano iliyopita kwenye wilaya hiyo ni pamoja na kujenga jengo la kujifungulia wajawazito katika hospitali ya wilaya, kituo cha afya Longoi na zahanati.

Serikali pia ilipeleka katika wilaya hiyo jumla ya Sh Bilioni 2.8 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba, Sh Bil 7.8 kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo, vilevile ujenzi wa maabara za kisasa, mabweni, madarasa na madawati.

Kukarabati shule kongwe za Machame Wasichana na Lyamungo, Sh Bil 3.4 zimegharamia miradi ya maji safi na salama katika vijiji mbalimbali, jumla ya Sh Bil 4.9 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami.

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli alisema, CCM itakapoendelea na miaka mingine mitano ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano atahakikisha viwanda vilivyokufa katika mkoa huo vinafufuliwa ili kuongeza ajira na kukuza biashara.

“Ndiyo maana tumeamua kufufua reli ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro hadi Arusha ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na malighafi. Tunataka maisha ya wananchi wa Kilimanjaro na mikoa mingine ya jirani yanakuwa mazuri,” alisema.

Awali, akizungumza na wananchi waliofurika katika viwanja hivyo jana, mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Saashisha Mafue alisema kaulimbiu yao kwa sasa ni Hai Mpya, Kilimo na Viwandakwa kuwa zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa jimbo hilo ni wakulima na wafugaji.

“Naomba nikushukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa uliyotufanyia katika taifa hili lakini kwa kipekee naomba niwashukuru wazazi wako kwa kukulea kwa maadili hadi unatuongoza ukiwa na uzalendo.

“Hapa Hai tunakuahidi tutakuchagua ka kura nyingi, tumeshazungukakata zote 17, vijiji 62, vitongoji 294 na tarafa 17 wananchi wote anaimba jina lako. Nikuambie wananchi wa Hai wanakupenda kweli,” alisema Mafue na kuongeza:

“Hakika umetufanyia mambo makuba ya kimaendeleo mbali ya kuwa katika kampeni zilizopita tulikuchanganyia magunzi, lakini wewe ni mtu mwenye upendo wa hali ya juu hukujali hayo.”

Akitaja baadhi ya fedha zilizoletwa katika jimbo hilo Mafue alisema jumla ya Sh Bil 12 zimepelekwa kwa ajili ya elimu bila malipo, sekta ya afya imepelekewa Bil 2.4, barabara zimepelekewa Bil 4 na ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya umegharimu Bil 1.4.

Jana Dk. Magufuli alikamilisha ziara yake ya kampeni katika Mkoa wa Kilimanjari iliyodumu kwa siku tatu, leo atakuwa na mkutano mkubwa katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini  Arusha.

…AZINDUA KIWANDA LITAKACHOZALISHA AJIRA 3000

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amezindua kiwanda cha Kilimanjaro Internationa Lather Industry kinachojengwa mkoani Kilimanjaro kitakachozalisha ajira 3000 za moja kwa moja pindi kitakapoanza uzalishaji.

Akizungumza katika hafla ya kuzindua kiwanda hicho kinachojengwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jaamii wa PSSSF na jeshi la Magereza, Rais Magufuli alisema alielekeza kijengwe mkoani humo kama hatua ya kufufua viwanda mkoani humo kikiwemo Kiwanda cha Karanga kilichokuwa kikizalisha bidhaa za ngozi.

Rais Magufuli alisema mbali na kuzalisha ajira za moja kwa moja, pia kitatoa fursa ya watu kujiajiri kwa kutoa huduma katika kiwanda hicho pamoja na kufanya biashara ya bidhaa za ngozi zitakazozalishwa.

Aliupongeza mfuko wa PSSSF kwa kuchukua hatua ya kuwekeza katika viwanda na kutoa wito kwa mifuko mingine kuiga mfano huo na kuachana na biashara za kujenga majengo “ambazo zimekuwa zikisababisha hasara.”

Rais Dk. John Magufuli, Waziri wa wa Mambo ya Ndani, George Simbachawe (Watatu kutoka kushoto) na baadhi ya Viongozi wakikata utepe katika Ufunguzi wa Kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro. Ufunguzi huo umefanyika jana , Mkoani Kilimanjaro

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here