FAO:Janga la nzige laendelea kuwatesa wakulima na wafugaji

0

Sana’a,Yemen

MAISHA  ya wakulima na wafanyakazi yameendelea kupata pigo kubwa kutokana na janga linaloendelea la nzige nchini Yemen ambao wamesambaratisha mazao, malisho ya mifugo na kuongeza shinikizo kwa maelfu ya watu ambao tayari wamechoshwa na miaka ya vita vinavyoendelea nchini humo limesema shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.

Katika Kijiji cha Hareeb jimbo la Ma’rin nchini Yemen mkulima na mfugaji  Musaeed Mubarak Ali Al-Gunaimi akitembelea shamba lake kuangalia uharibifu uliofanywa na nzige hao wa jangwani anasema wameshambulia mazao yote ya wakulima kuanzia matunda, vitunguu, ufuta, mpunga na hata mitende na kusababisha hasara kubwa kwao. Na kana kwamba hilo halitoshi ,

“Makundi ya nzige hao yameshambulia mashamba na kumaliza mazao yote na sasa kilichosalia yatakula chakula cha mifugo ambacho tunatumia kulisha kondoo wetu”

FAO  inasema imekuwa ikiisaidia wizara ya kilimo na umwagiliaji ya Yemen kupambana na nzige hao wa jangwani kwa operesheni mbalimbali ikiwemo za kiuifundi na mafunzo kwa timu za mashinani. Lakini maeneo yaliyoathirika ni mengi.

Hussain Mohamed Abdullah Al-Zubaid ni mkulima kutoka jimbo la Tarim anasema,“Nzige wamekula kila kitu ndani ya siku nne na hawakuacha chochote isipokuwa vijiti

Msaada wa FAO ni pamoja na zaidi ya lita 14,850 za dawa za kuulia wadudu na mafunzo kwa watu 393 ambao watahusiska na masuala ya afya, usalama na mazingira wakikabiliana na nzige hao.

Msaada ambao umepokelewa kwa mikono miwili na wakulima na wafugaji wa Yemen kama anavyosema mkurugenzi mkuu wa kituo cha ulinzi wa mazao na wkulima Yasir Mohammed Saleh Ali,

“Tumeathirika sana kwa kukosa uwezekano na msaada wa fedha, hata hivyo tunaishukuru FAO kwa juhudi zake na kituo cha ulinzi wa mazao na wakulima kwa kuwezesha zoezi hili. Mungu akijalia tutaanza jukumu  na kusaidia tuwezavyo. Bado tunahitaji timu ya watu zaidi kwa sababu hatujaweza kushugfhulikia eneo lote sababu tuna magari mawili tu hapa na moja ni la kufanya ukaguzi.”

Kwa mujibu wa FAO kutokana na vita sio maeneo yote yanayoweza kufikiwa na msaada kwa sababu ya usalama hali ambayo inawapa nzige fursa ya kuzaliana na kuongezeka na hivyo kuongeza shinikizo kwa wakulima na wafugaji  nchini humo.

Katika nchi za Afrika Mashariki  wadudu hao hatari kwa mazao waliingia  mwezi Februari mwaka huu  na kuanza kushambulia mazao nchini Kenya.

Baadaye waliingia nchini Uganda ambapo Maafisa wa Uganda walisema kwamba nzige wameingia nchini humo kutoka Kenya, na kuthibitisha hofu zilizowasilishwa na maafisa wa UN kwamba wadudu hao waharibifu wataendelea kuenea katika eneo la Afrika mashariki.

Wadudu hao walidaiwa kupatikana katika eneo la mashariki la wilaya ya Amudat inayopakana na Kenya,Afisa wa kilimo katika wilaya ya Amudat awali alidaiwa kusema kwamba wadudu hao walikuwa umbali wa kilomita 4 kutoka katika mpaka katika eneo linalojulikana kama Kiwawa nchini Kenya.

Kundi la nzige limeharibu eneo kubwa la mashamba na linatishia kuangamiza chakula katika eneo la Afrika mashariki.

Kenya tayari imeripoti mlipuko mbaya zaidi wa nzige katika kipindi cha miaka 70. Mabilioni ya wadudu hao tayari wameharibu makumi ya maelfu ya ekari za mimea nchini humo.

Mlipuko wa wadudu hao uliovunja rekodi pia uliripotiwa nchini Ethiopia na Somalia. Wadudu hao pia wameshambulia maeneo ya taifa la Sudan, Djibout na Eritrea.

Shirika la usalama wa chakula na kilimo katika Umoja wa mataifa FAO limetaja uvamizi huo wa nzige Afrika mashariki kuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25.

Nchini Somalia, serikali ilitangaza janga la dharura kutokana na uvamizi wa wadudu hao waharibifu.

Ilisema kwamba mlipuko huo ulikuwa unatoa tishio kwa hali mbaya ya ukosefu wa chakula. Ndege zimekuwa zikimwaga dawa za wadudu ili kudhibiti idadi ya nzige hao

Lakini maafisa wamesema kwamba wana fedha chache na vifaa kukabiliana na wadudu hao katika maeneo yalioathirika.

Maafisa wa Umoja wa mataifa wanasema kwamba wana wasiwasi kwamba wadudu hao wanaweza kusambaa hadi Sudan kusini.

Wanakadiria kwamba takriban dola milioni 76 zinahitajika kwa sasa kuimarisha juhudi zinazolenga kuzuia kuenea kwa wadudu hao Afrika Mashariki.

Nzige hao wa jangwani ambao wana urefu wa kidole cha mwanadamu huruka kwa makundi makubwa makubwa wakitafuta lishe.

Shirika la IGAD , limeripoti kwamba kundi moja la nzige huenda linashirikisha wadudu zaidi ya milioni 150 kwa mraba.Limesema kwamba wadudu hao husafiri kupitia upepo na wanaweza kusafiri kwa zaidi ya kilomita 150 kwa siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here