Fahamu matukio makubwa yaliyofutwa ama kuahirishwa kutokana na corona

0

NA MWANDISHI WETU

Mwaka 2020 ambao umefika ukingoni, utabaki katika historia ya dunia kama mwaka wa janga la virusi vya corona. Japo mlipuko huo ulianza mwishoni mwa 2019, mwaka 2020 ndiyo hasa dunia ilipitia katika machungu yake.

Hali ilivyo sasa, ukingoni mwa 2020 ni ya matumaini zaid baada ya kinga kadhaa kuonekana kuwa na ufanisi. Tayari kinga aina ya Pfizer/BioNTech imeshaanza kutolewa nchini Uingereza na mataifa kadhaa duniani yapo mbioni kuanza kutoa kinga kwa wananchi wake. Shughuli nyingi za kiuchumi, kisiasa na hata michezo zinaendelea, japo bado hazijarejea katika kiwango cha kabla ya janga hilo.

Hata hivyo miezi ya mwanzoni na mpaka kufikia katikati ya mwaka, hali ilikuwa mbaya, idadi ya maambukizo na vifo ikipanda kila uchao, milango ya kutangamana baina ya watu na mataifa ikawa inafungwa mmoja baada ya mwengine.

Kutokana na hali hiyo, matukio kadhaa, madogo na makubwa yaliathirika kwa viwango tofauti, baadhi yakifutwa kabisa, mengine yakibadili utaratibu wa uendeshaji na huku mengine yakiakhirishwa. Haya ni baadhi ya matukio makubwa yaliyoathirika na athari zake.

Uchaguzi wa Ethiopia na ‘mzozo’ wa Tigray

Mwezi Agosti mwaka huu ilipangwa kufanyike uchaguzi nchini Ethiopia. Uchaguzi huu ilitarajiwa kuwa utotoa kipimo halisi cha kukubalika kwa Waziri Mkuu kijana Abiy Ahmed kwa raia wa nchi hiyo.

Abiy aliingia madarakani mwezi Aprili 2018, na punde tu mambo yakaanza kubadilika. Ethiopia ambayo ilikuwa na jina baya la kuminywa kwa demokrasia, maandamano ya upinzani wa jamii ya Waoromo na mgogoro wa mpaka baina yake na Eritrea yote hayo yakapatiwa ufumbuzi. Wafungwa wa kisiasa wakaachiwa, maandamano yakaisha, na baraza la mawaziri likapata uwakilishi mkubwa wa wanawake.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2019, mapinduzi hayo yakampatia tuzo ya amani ya Nobel.

Hatua iliyokuwa ikisubiriwa baada ya hapo ikawa ni uchaguzi mkuu, hata hivyo virusi vya corona vikatapakaa dunia nzima, na kufikia Mwezi Machi mwaka huu virusi hivyo vikatangazwa kuwa janga la dunia. Serikali Kuu nchini Ethiopia kuakhirishwa kwa kura ya mwezi Agosti kutokana na janga hilo.

Serikali zote za majimbo nchini humo, isipokuwa kwa jimbo la Tigray ziliridhia kuakhirishwa kwa uchaguzi. Mwezi Septemba, jimbo hilo ambalo lipo chini ya chama cha TPLF likafanya uchaguzi ambao Abiy na serikali ya Addis Ababa ilisema kuwa ni wa haramu.

Abiy Ahmed amebadilisha Ethiopia – lakini migongano ya ndani kwa ndani hususani ya kikabila bado ni kizingiti kikubwa

Uchaguzi huo, ukachochea zaidi mgogoro baina ya TPLF na serikali ya Abiy. Toka awali chama cha TPLF kilionekana kutokuunga mkono na kuridhishwa na mapinduzi ya kimfumo ambayo yalikuwa yakiendeshwa na Abiy, hususan kuleta suluhu na nchi ya Eritrea na kuunganisha vyama vya kikabila vilivyounda serikali chini ya muungano wa ERDF toka 1991 kuwa chama kimoja cha siasa cha PP.

TPLF, ilikuwa ni mwanachama kinara wa ERDF na toka mwaka 1991 ndiyo waliokuwa vinara kwenye serikali ya Ethiopia. Abiy anatoka katika jamii ya Oromia ambayo ndiyo ilikuwa ikiongoza maandamano dhidi ya serikali. Mabadiliko aliyokuwa akiyatekeleza hayakuwapendeza TPLF ambao waliona kuwa nguvu na ushawishi wao umepotea, huku Abiy kwa upande wa pili akiona kuwa matendo ya TPLF yalikuwa yakionesha dharau dhidi ya utawala wake.

Hali ya mambo baina ya pande hizo mbili ilichacha zaidi Novemba 4, baada ya serikali kuu kutuhumu wapiganaji wa chama cha TPLF kushambulia kambi ya jeshi la taifa katika eneo la Tigrinya kwa nia ya kupora silaha. Huo ukawa mwanza wa vita ya wenyewe kwa wenyewe baina ya pande hizo, ambapo kufikia wiki ya kwanza ya Disemba bwana Abiy alitangaza kuwa serikali kuu ilikuwa ‘imeshalikomboa’ jimbo la Tigray kutoka kwa waasi wa ‘TPLF’.

Laiti uchaguzi usingeakhirishwa kutokana na mlipuko wa corona, yawezekana mgogoro wa kisisasa nchini Ethiopia usingefikia hali mbaya ambayo imeshuhudiwa mwishoni mwa mwaka huu.

Hija na maadhimisho ya pasaka

Moja ya matukio makuu katika kalenda za dini kubwa zaidi mbili duniani Uislamu na Ukristo ni Hija ambayo mwishowe hupatikana siku kuu ya Eid al-adha (ama idi ya kuchinja) na siku kuu ya Pasaka ambayo ni kumbukumbu ya kusulubiwa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Ibada ya Hija ni moja ya nguzo tano za usilamu na ni lazima kwa kila mwenye uwezo wa kifedha na afya kuitekeleza walau mara moja katika maisha yake. Ibada hiyo hufanyika nchini Saudi Arabia katika miji mitakatifu ya Makka na Madina na katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikifanywa na mpaka watu milioni mbili kwa mkupuo.

Mwaka huu, ibada hiyo iliadhimishwa mwishoni mwa mwezi Julai mpaka mwanzoni mwa Agosti, hata hivyo ni watu 1000 tu ndio walioruhusiwa kuitekeleza na si mamilioni kama ilivyozoeleka. Hatua hiyo ilifikiwa na mamlaka za Saudia ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi ikizingatiwa mahujaji hutoka kila pembe ya dunia.

Matukio kadhaa ya kumbukizi ya kidini hufanyika wakati wa pasaka kwa takribani juma moja, ambapo Wakristo wa madhehebu mbalimbali duniani hujumuika makanisani na majumbani kuabudu na kusherehekea katika mwezi wa Aprili. Kipindi hicho kwa mwaka huu ndio ilikuwa kilele cha maambukizi katika mataifa mengi duniani.

Kutokana na tishio hilo, makanisa mengi duniani yalikuwa yamefungwa huku ibada zikiongozwa kwa njia ya mtandao wa intaneti. Katika kanisa la Mtakatifu Petro jijini Vatican, Papa Francis aliongoza ibada bila ya kuwepo waumini katika kanisa hilo kubwa lenye uwezo wa kupokea maelfu ya watu. Ibada hiyo ilirushwa mbashara ili mamilioni ya waumini wa kanisa katoliki kuifuatilia wakiwa nyumbani.

 Olimpiki

Haya ndiyo mashindano makubwa zaidi ya michezo ulimwenguni, na mwaka huu yalipangiwa kufanyika nchini Japani mwezi Juni na Agosti.

Dalili za kushindikana kwa michuano hiyo zilishaonekana toka mwishoni mwa mwezi wa pili, lakini mpaka kufikia katikati mwa mwezi Machi maafisa kutoka nchi ya Japani ambayo ndio waandaaji wa michuano hiyo pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) walikuwa wakisisitiza kuwa michuano itaendelea kama ilivyopangwa awali.

Mataifa kadhaa ikiwemo Canada, Australia na Uingereza yalitishia kujitoa katika mashindano hayo endapo yangefanyika mwaka huu. Machi 24, Japani na IOC wakatangazwa kuhirishwa kwa michuano hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa sasa masikio ya wapenzi wa michuano hiyo yanaelekezwa Julai 2021. Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Kenya ndio imekuwa ikiwakilisha vyema, na watu wengi nchini humo huyasubiria mashindano hayo kwa hamu kubwa. Uganda wao hujitokeza mara moja moja huku Tanzania ikiwa msindikizaji, mara ya mwisho taifa hilo kushinda medali ilikuwa miaka 40 kamili iliyopita mwaka 1980. Suleiman Nyambui na Filbert Bayi wakishinda medali za fedha.

Mwaka 2016, jijini Rio Brazil Kenya ilinyakua jumla ya medali 13, kati ya hizo sita zikiwa za dhahabu. Mwaka 2012 jijini London Kenya iliibuka na medali 11, mbili zikiwa za dhahabu.

Na mwaka huu pia, kapu la Kenya la medali linategemewa kuendelea kunona.

Bingwa asiye mpinzani Eliud Kipchoge anapigiwa upatu kuitetea medali yake ya dhahabu katika mbio za marathon aliyoishinda jijini Rio 2016.

Euro 2020

Ilikuwa iwe ni mara ya kwanzan katika historia kwa mashindano ya timu za taifa za kandanda za Ulaya yatafanyika katika nchi 12 tofauti.

Hii ni michuano ya pili kwa ukubwa ya kandanda duniani baada ya Kombe la Dunia na hufanyika kila baada ya miaka minne. Mechi ya ufunguzi ilipangwa ifanyika jijini Roma kati ya Italia na Uturuki huku fainali ikipangiwa kuchezwa Wembley, Uingereza.

Mfumo huo ulipendekezwa ili kuwa kama alama ya kusherehekea miaka 60 mashindano hayo. Hata hivyo, katikati ya mwezi Machi, waandaaji wa michuano hiyo UEFA walitangaza kuikhirisha kwa mwaka mmoja mpaka mwakani, ili kuruhusu mapambano dhidi ya janga hilo kufanyika.

Sasa mashabiki wa kandanda wanasubiria kwa hamu michuano hiyo kufanyika mwakani na ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa, timu nne zilizocheza nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 Croatia, Uingereza, Ubelgiji na Ufaransa zinatoka Ulaya.

Mwaka 2016, timu ya taifa ya Ureno ambayo haikupigiwa chapuo na wengi iliwaacha mahabiki midomo wazi kwa kunyakua kombe hilo. Inaelekea haya ndiyo yatakuwa nashindano ya mwisho ya Euro kwa nyota wao Cristiano Ronaldo mwenye miaka 34, swali ni kuwa ataweza kuiongoza timu yake kutetea ubingwa?

CHANZO: BBC

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here