Dk. Shein, Watendaji Serikali waagana wakisheherekea mafanikio lukuki

0
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto), akipokea zawadi iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Hai Ussi (GAVU), katika sherehe maalum mafanikio ya miaka 10 ya Uongozi wake     iliyoandaliwa kwa Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walipomuaga rasmi jana katika  viwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar.

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameagana na Watendaji aliowateua katika nyadhifa mbali mbali Serikalini na kusema kwamba hafla hiyo ni kielelezo cha mafanikio katika kuendeleza na kudumisha demokrasia na utawala bora nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo jana katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar katika hotuba ya kuagana na Watendaji aliowateua katika nyadhifa mbali mbali  katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa mfumo mzuri wa kisheria wa kubadilishana, kupokezana na kuacha madaraka ni miongoni mwa mambo yaliyoipatia sifa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar duniani kote.

Alisema kuwa viongozi wa Tanzania wamejijengea sifa ya kuacha, kukamilisha na kupokezana madaraka  kwa nafasi mbali mbali kwa hali ya salama na utulivu.

Aliongeza kuwa suala la kubadilishana madaraka au kuachia kwa hiari ili kutoa nafasi kwa wengine katika ngazi mbali mbali ni utamaduni uliojengeka hata kwa chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Rais Dk. Shein alisema kuwa viongozi wote hao akiwemo yeye mwenyewe wanawajibika kwa wananchi wa Zanzibar kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni yao hivyo alisisitiza haja ya kuwatumikia wananchi iapsavyo.

Alieleza kuwa jambo ambalo amekuwa akilisisitiza kwa kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake ni kuwataka watumishi wa umma wafahamu jukumu lao kubwa la kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mipango iliyopangwa ya Maendeleo ikiwa ni pamoja na mafanikio ya Dira ya Maendeleo 2020, Mipango ya Kimaendeleo ya Kimataifa.
Alisema kuwa kasi ya maendeleo iliyofanywa na Awamu ya Saba imetokana na kasi za Awamu zilizopita ambapo mafanikio yameweza kupatikana ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa uchumi kwa asilimia 7.

Alieleza kuwa ndani ya miaka 10, Sheria 128 zimetungwa na kuwa Sheria za Zanzibar jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar ambapo katika Sheria hizo mbili miongoni mwao ni Sheria ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi na ile Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma.

Rais Dk. Shein akinukuu Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwenye Ibara ya 28 kifungu cha 3, ambacho kinasema kwamba “Bila ya kuathiri chochote kilichomo katika kifungu hiki cha Katiba hii hakutakuwa na mtu yoyote ataechaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja”.

Alitoa pongezi kwa Watendaji wote aliowateua kwa kufanya kazi vizuri na kuweza kuwasaidia wananchi na kusema kuwa anathamini juhudi zao hizo zilizopelekea Zanzibar kupata mafanikio.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mara nyingi inapofanywa safari jambo la kwanza linaloombwa ni  kujaalia safari ya salama na inapofikwa safari hiyo jambo linalofuata ni kutoa shukurani kwa kufika salama na kusema kuwa safari ya miaka 10 ni ndefu.

Alisema kuwa shughuli hiyo ya kuagana inatoa furaha kubwa akikumbuka kwamba anawaaga watendaji hao wakiwa wamefanya mambo mengi mazuri kwa pamoja kwa ajili ya kuwatumikia wananchi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here