Dk. Ndugulile: Kituo cha kuhifadhi data ni salama

0
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akijadiliana jambo na Meneja wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data, Godfrey Mpangala (wa pili kushoto) wakati wa ziara yake kituoni hapo, Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri, Mhandisi Kundo A. Mathew na wa tatu kushoto ni Katibu Mkuu, Dkt.Zainab Chaula, wote wa Wizara hiyo

  >>Awapa onyo wanahujumu miundombinu TTCL 

NA AZIZA MASOUD,DAR ES SALAAM

KUMEKUWA  na changamoto kubwa yakuhifadhi  taarifa za watu binafsi,taasisi na mashikirika mbalimbali nchini jambo ambalo linalosababisha  baadhi ya watu kutokuwa na uhakika wa uhifadhi wa kumbukumbu zao katika maeneo mbalimbali.

Ili kuondoa tatizo hilo na kuhakikisha  watu wanahifadhi taarifa zao vizuri serikali kupitia Shirika la Mawasiliano nchini(TTCL)  ilifungua kituo  cha mawasiliano nchini lengo likiwa ni kuhakikisha  taasisi na watu mbalimbali wanakuwa na kumbukumbu zao.

Kutokana na hali hiyo serikali imeendelea kuzihimiza taasisi hasa za serikali  kuhakikisha wanahifadhi  taarifa zao katika kituo hicho.

Hivi karibuni  Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk.Faustine Ndugulile amehimiza taasisi za Serikali kutumia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) kuhifadhi taarifa zao kwa kuwa ni sehemu salama, ina miundombinu na mifumo ya TEHAMA ya kisasa na ina wataalamu wabobezi na ina nafasi ya kutosha kwa ajili ya kupangisha mifumo.

Dk. Ndugulile ameyasema hayo alipofanya  ziara yake ya kutembelea NIDC, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo Mathew, Katibu Mkuu, Dk. Zainabu Chaula, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba na watendaji wa Wizara hiyo na kubaini kuwa ni taasisi 84 tu za Serikali zinatumia NIDC kati ya taasisi 149 zinazohifadhi taarifa zake kwenye kituo hicho

Dk.Ndugulile amezikumbusha taasisi za Serikali kuzingatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alilolitoa alipotembelea NIDC kuzindua Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato (electronic Revenue Collection System – eRCS) mwaka 2017 ambapo umeiwezesha NIDC kuongeza makusanyo ya mapato yake kutoka Sh Bilioni 1.4 mwaka 2019 na kufikia shilingi bilioni 2.76 mwaka 2020

Naye Naibu Waziri, Mhandisi  Mathew ameipongeza NIDC kwa kutengeneza mifumo mbali mbali ya TEHAMA ambayo inaiwezesha Serikali kuongeza makusanyo ya mapato na kurahisisha  maisha kuendana na mahitaji ya wananchi ikiwemo kulipa tiketi ya mabasi ya njia ya mtandao; kuweka mafuta kwenye gari; kulipa kiingilio kwenye uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa; usafiri wa kivuko cha Kigamboni; usajili wa leseni BRELA;  na maegesho ya magari uwanja wa ndege wa Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo A. Mathew akizungumza na wafanyakazi wa NIDC (hawapo pichani).

Katibu Mkuu, Dk. Zainab Chaula amewaeleza watendaji wa NIDC washirikiane kwa karibu na wataalamu wa Wizarani ili kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kuwahudumia wananchi kwa kutumia TEHAMA ili kuokoa muda wao kutafuta huduma za Serikali badala yake watumie kufanya kazi na kuongeza uzalishaji mali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akizungumza na wafanyakazi wa NIDC (hawapo pichani).

Meneja wa NIDC, Geofrey Mpangala amesema kuwa wateja wanaotumia kituo hicho wamepunguza gharama za uendeshaji na uwekezaji kwenye taasisi zao kwa kuwa hawajengi miundombinu na mifumo ya TEHAMA; wateja wanapata viwango vya juu vya data yenye kasi na uhakika wa usalama wa data zao na huduma zinatolewa kituni hapo kwa saa 24.

Katika hatua nyingine  Dk.Ndugulile alitoa  mwezi mmoja kuhakikisha wizara na taasisi za serikali zinazodaiwa na Shirika la Mawasiliano la Simu TTCL kulipa madeni yao ambayo ni zaidi ya Sh Bilioni 30 kabla ya maene hayo hayajasitishiwa huduma.

Dk.Ndugulile ametoa kauli hiyo alipofanya ziara katika shirika hilo ambalo lipo chini ya wizara hiyo mpya kwa lengo la kufahamiana na kusikiliza changamoto zilizopo

Amesema taasisi na wizara hizo ambazo zipo zaidi ya 20 zinapaswa kuandikiwa barua na Mkurugenzi ambazo zitawakata kila mmoja kulipa deni analodaiwa ifikapo Januari 31 mwakani.

“Taasisi zinazodaiwa zote zinapaswa kulipa fedha hizo zinazotokana na huduma wanayopatiwa ifikapo Januari 31 baada ya hapo nitachukua hatua yakusitisha huduma ikiwemo kukata mawasiliano katika maeneo husika,”amesema Dk.Ndungulile.

Amesema ni muhimu wizara na taasisi hizo kuzingatia suala hilo kwakuwa shirika linatumia gharama kubwa kujiendesha ikiwemo kuendesha mkongo wa Taifa.

Mbali na hilo Dk.Ndugulile pia amesema serikali imebaini hujuma zinazofanyika katika mkongo wa Taifa za baadhi ya watu kuiba nyama na kwenda kuyeyusha kutengeneza madini ya kopa jambo ambalo linaosababishia shirika hasara.

“Kuanzia sasa naenda kuongea na vyombo vya ulinzi na usalama kuwaelekeza ikitokea mtu yoyote kakamatwa na hizi nyaya ana kopa ambayo haijulikani chanzo chake ataingia kwenye orodha ya wahujumu uchkumi,”amesema Dk.Ndugulile.

Pia Dk.Ndungulile ametoa tahadhali kwa watia huduma za mtandao ambao wanahujumu mitambo ya TTCL ili isifanye kazi vizuri na kuahidi kuwashughulikia.

“Kampuni zinazoihujumu TTCL nazijua na sitozitaja,nawapa taarifa tunajua wanachofanya hizi salam ziwafikie tutawachukulia hatua kali,”amesema Dk. Ndugulile.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL  Kindamba aliahidi kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Waziri na kuwataka wafanyakazi wa shirika hilo kufanya kazi kwa bidii na kuacha mazoea.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dk. Faustine Ndugulile akimsikiliza Mkurugenzi wa TTCL, Waziri Kindamba alipofabyw ziara makao makuu ya Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here