Dk. Mwinyi, Maalim Seif kudumisha maridhiano

0

NA MWANDISHI WETU

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad wamefungua ukurasa mpya wa maridhiano na kuahidi kushirikiana katika kuyadumisha.

Hayo yamedhihirika katika hotuba zao jana katika hafla ya uwapisho wa Makamu wa Kwanza wa Rais ambapo wote waligusia umuhimu wa kusahau historia ya siasa za uhasama na chuki na kujenga Zanzibar yenye mshikamano kwa maslahi ya Wanzanzibar.

Katika hotuba yake Dk. Mwinyi alisema atajitahidi kuhakikisha anajenga na kudumisha maridhiano kwa maslahi mapana ya Zanzibar huku akiahidi kushirikiana na makamu wa kwanza wa rais, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Novemba 2 mwaka huu niliapa pale uwanja wa Amani kuwa rais wa awamu ya nane wa Zanzibar. katika kiapo changu pamoja na mambo mengine niliapa kulinda na kuongoza nchi yetu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.”

“Katiba yetu kifungu cha 9 (3) inaelekeza muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utakuwa wa umoja wa kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanyika kwa utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja na lengo la kufikia demokrasia. Kifungu cha 39 (3), kinanitaka kumteua makamu wa kwanza wa rais kutoka kwa chama kilichopata nafasi ya pili.”

Dk Mwinyi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) alisema, “yale yaliyo ndani ya mamlaka na uwezo wangu nitayatekeleza bila ajizi na kwa kuanzia nimetekeleza matakwa ya katiba ya kuwafikia wenzetu wa ACT na kuwakaribisha kuunda Serikali.”

“Kwa mamlaka niliyopewa kwenye kifungu cha 66 cha katiba ya Zanzibar, jana (juzi) niliwateua Nassor Ahmed Mazrui na Omar Said Shabaan kuwa wawakilishi kutoka miongoni mwa nafasi 10 nilizopewa za kuteua wajumbe wa baraza la wawakilishi,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema atashauriana na Maalim Seif kuhusu kujaza nafasi zilizobaki katika baraza la mawaziri na namna bora kuendesha Serikali ya umoja wa kitaifa.

Dk Mwinyi alisema maridhiano ya kweli yanajengwa kwa mambo matatu ambayo ni dhamira, kuvumiliana, kustahimiliana na kusahau yaliyopita na kujenga utamaduni wa kuaminiana.

“Sisi viongozi kila wakati hatuna budi kuzingatia maslahi ya wananchi ndiyo jambo la msingi. Tofauti zetu ndogo au kubwa zisiwe kikwazo kwa maendeleo ya wananchi.”

“Sote tuwe kitu kimoja na tuunge mkono juhudi hizi zenye lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Maridhiano yetu yatategemea utayari wa vyama vyetu na wananchi kuzipa kisogo tofauti na kuyatazama matumaini yaliyo mbele yetu mimi na Maalim Seif tumeonyesha utayari nyie mridhiane kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.

Kwa upande wake Seif alisema sababu iliyowafanya kukubali kuunda Serikali ya Umoja wa      Kitaifa ni imani yao kwa Dk Mwinyi, maneno yake, vitendo na ishara ambazo ziliwashawishi kuona ana nia njema na dhamira safi ya kuibadilisha Zanzibar.

“Tumeona wewe ni mtu tunayeweza kufanya naye kazi, kusikilizana na tumekupa nafasi udhibitishe nia yako njema ambayo ndiyo iliyotufanya tutangulize nchi kwanza licha ya yote yaliyotokea,” alisema Seif

Alisema chama chake kimekubali ashiriki kuunda Serikali kusaidia azma ya kutibu majeraha ya Zanzibar na kuyastawisha maridhiano.

Alisema lengo la maridhiano si tu kuwa na mfumo shirikishi bali yalilenga kuondoa kabisa siasa za mivutano, zilizoitawaliwa na chuki, uhasama na visasi ambavyo kwa njia moja au nyingine vimekwamisha ustawi wa Zanzibar kwa muda mrefu.

“Uchaguzi mkuu uliopita na changamoto zilizojitokeza zimetufunua macho kuwa majibu ya kisheria na kikatiba pekee hayatoshi kutufikisha katika matamanio yetu ya maridhiano tunao wajibu wa kutafuta jawabu pia kutafuta mwafaka wa kijamii,” alisema Seif na kusisitiza;

“Zanzibar iliyogawika haiwezi katu kupiga hatua ya maendeleo. Maridhiano, amani, utulivu ndiyo majibu ya kuhuisha Zanzibar kutoka ilipo sasa kwenda kwa Zanzibar iliyopiga hatua kimaendeleo.

“Kwasababu ya mwelekeo huu ndiyo maana chama cha ACT Wazalendo na mimi mwenyewe binafsi nimekubali kuingia kwenye umoja wa kitaifa ili kuijenga Zanzibar Mpya,” alisisitiza.

Alisema yeye na Chama chake wanaamini wajibu wa mwanzo wa Serikali ya awamu ya nane utakuwa kuwaungaisha wananchi wa Zanzibar kuwa wamoja.

“Nikuhakikishie juu ya dhamira yetu safi, mimi na wenzangu ya kufanya kazi na wewe kwa manufaa ya Zanzibar yetu. Nikupongeze wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, niwapongeze mawaziri wote na wakuu wa mikoa waliobahatika kuteuliwa.

“Nitoe wito kwa Zanzibar wote walioko ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkuno wa maridhiano.Tumeze machungu yaliyotokana na uchaguzi. Historia yetu imejaa kila aina ya majeraha ni wakati wa kuzika historia hiyo na kushikamana ili kujenga Zanzibar yetu. Maridhiano yatafungua milango ya kuwezesha Serikali kuchukua hatua za marekebisho na kujenga upya pale palipovunjwa, palipovurugwa na pale palipoharibika na pale palipokosewa,”alisema Seif.

“Nitakupa mashirikiano, mawaziri na wakuu wa mikoa wote na yeyote yule ambaye atahitaji ushauri wangu milango yangu iko wazi,” alihitimisha Seif.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here