Dk. Mwinyi awataka wazanzibar kuunga serikali ya umoja wa kitaifa

0
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislam baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid Jibri Mkunazini Jijini Zanzibar leo disemba 11, 2020.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili iwaletee maendeleo.

Alhaj Dk. Hussein aliyasema hayo leo huko Masjid Jibril, Mkunazini Jijini Zanzibar wakati akitoa salamu kwa Waumini wa dini ya Kiislamu mara baada ya kumaliza sala ya
Ijumaa.

Alieleza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeshaundwa na viongozi wamekubaliana
kuweka tofauti zao ili kuwaunganisha wananchi wote wa Unguja na Pemba bila ya
kujali imani za kidini itikadi zao za kisiasa na wamekubali kuwa wamoja kwa azma ya
kuijenga nchi yao.

Pamoja na hayo, alisema kuwa Mwenyezi Mungu amekubali dua za Waumini na vyama
vimekubali kushiriakiana kwani ilifikia wakati wa uchaguzi watu wanapoteza amani, wanafarakana, mume anamuacha mke kwa sababu za itikadi za kisiasa, watu hawazikani, hawasali pamoja mambo ambayo ni kinyume na maamrisho ya dini ya
Kiislamu.

Aidha, alisema kuwa dini ya Kiislamu inawataka watu wote wawe wamoja, washikamane, wapendane na kuwaomba Waumini kwamba Serikali ya Umoja wa
Kitaifa iachwe ifanye kazi ya kuleta maendeleo na isiwe na kazi ya kuwaunganisha watu kwa mifarakano yao.

Alisema kuwa si wote waliofurahia maridhiano hayo, lakini bado kuna nafasi ya
kuwaelimisha watu na kusema kuwa dini ya Kiislamu inawataka watu kuwa wamoja hivyo, watu wote wenye kinyongo wawe kitu kimoja katika kuijenga nchi na kutokana
na dhamira iliopo yale yote yaliyoahidiwa wakati wa Kampeni yatatekelezwa.

aAliongeza kuwa, umoja wa Kitaifa unahitajika na tayari umeshapatikana katika ngazi za juu ya kujenga Serikali lakini pia, unahitajika kupatikana kwa wananchi wote ili kuweza kutimiza majukumu yaliyo mbele.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa hivi sasa kuna kila dalili ya maridhinao baina ya
wananchi na kumuomba Mwenyezi Mungu kuwawezesha wananchi wote wawe kitu
kimoja ili waweze kujiletea maendeleo na mafanikio makubwa katika nchi yao.

Kwa maelezo yake Alhaj Dk. Mwinyi alikwenda msikitini hapo akiwa mgombea wa
Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupewa fursa ya kuzungumza ambapo
aliwaomba Waumini kuhakikisha amani iliyopo inalindwa wakati wote wa uchaguzi.

Alisema kuwa MwenyeziMungu amekubali dua za Waumini hao na kupelekea nchi kuwa
na amani na utulivu wakati wote sambamba na kuendelea kuwepo hadi hivi leo kwani
yote yaliyoahidiwa wakati wa Kampeni hayatekelezeki bila ya kuwepo kwa amani na
umoja baina ya wananchi.

Alisema kuwa baada ya amani kuwepo kinachotakiwa hivi sasa ni umoja, mshikamano, maelewano, maridhiano na mapenzi miongoni mwa wananchi wote kwani ndivyo dini ya Kiislamu inavyosisitiza.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa bado kuna madhila katika jamii, rushwa, udhalilishaji
wa watoto, watu kunyanganywa haki zao mambo ambayo atahakikisha anayaondoa
kwa uwezo wa MwenyeMungu na kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi.

Alisema kuwa ushirikiano ni lazima katika kupambana na madhila hayo ambapo kwa
upande wa kadhia ya udhalilishaji jambo hilo ni rahisi kupambana nalo kwani wanaofanya vitendo hivyo wamo katika jamii lakini kuna kila aina ya kufifisha ili wanaohusika wasifikishwe katika vyombo vya sheria.

Maeneo mengine ambapo kesi zinafifishwa alieleza kuwa ni katika vituo vya Polisi,
utaratibu wa kisheria ambapo pia katika jamii wamekuwa wanawaficha na wamo
wanaopatana na wadhalilishaji ambao hulipwa fedha ili wanyamaze huku akisisitiza
kwamba ni lazima madhila hayo yaondoke na kufanyiwa kazi kwa nguvu zote.

Aliushukuru uongozi wa Masjid Jibril na kuwaahidi Waumini wa dini ya Kiislamu
kwamba kazi yake kubwa itakuwa ni kuwaunganisha wananchi wote wa Zanzibar ili lao liwe moja.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here