Dk. Mwinyi akutana na viongozi wa kanisa la TAG

0
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, TAGk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Barnanas Weston Mtokambali alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kutowa pongezi zake kwa Rais na (kulia kwa Askofu) ni Rev. Dikson Kaganga, Askofu wa Jimbo la Zanzibar, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo Disemba 11/, 2020. (Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ameupongeza uongozi wa Kanisa la ‘Tanzania Assemblies of God’ (TAG)
kwa kuendelea kuhubiri amani na kuliombea Taifa wakati wa uchaguzi, kabla na
baada uchaguzi.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na
uongozi wa Kanisa hilo ukiongozwa na Askofu Mkuu wa Tanzania Barnabas Weston Mtokambali akiwa amefuatana na Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Dikson Kaganga, uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu 2020.

Katika maelezo yake, Dk.Mwinyi ametoa shukurani kwa uongozi huo kwa ujio wao
sambamba na pongezi na maneno ya hekima waliyayatoa kwa Rais.

Dk.Mwinyi pia ametoapongezi kwa uongozi huo wa Kanisa la TAG kwa ushirikiano
uliotoa katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu
wa mwaka huu 2020 katika kuliombea amani Taifa.

Amesema kuwa katika kipindi cha Kampeni aliweza kukutana na waumini wa dini ya
Kikristo wa madhehebu mbali mbali na kuzungumza nao ambapo pia na wao walieleza
changamoto walizonazo ambapo aliahidi kuzifanyia kazi.

Dk.Mwinyi ametoa shukurani kwa Kanisa hilo kwa kuunga mkono
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kwamba Serikali anayoiongoza
itashirikiana nao kwa kuthamini huduma inazozitoa kwani mbali ya huduma
za kiroho pia, limekuwa likichangia katika sekta ya afya, elimu na maji na nyenginezo.

Amesema kuwa maombi yote ya wananchi yameweza kukubaliwa na Mwenyezi Mungu na
hivi sasa tayari kuna maridhiano ambapo lengo lake ni kuondoa kasoro katika kada za
kisiasa hivyo, aliwanasihi waumini wote kuendelea kuliombea Taifa.

aidha Dk.Mwinyi amempongeza Askofu Mtokambali, kwa nafasi yake ya uongozi aliokuwa nayo kwa Tanzania na pia kuwa kiongozi mkuu wa Makanisa yote 48 ya TAG barani Afrika, Mjumbe wa Halmashauri ya Kanisa hilo katika makanisa 150 duniani na kueleza kuwa yeye akiwa Rais yuko tayari kushirikiana nae na milango yake iko wazi.

Mapema Askofu  Mtokambali alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa niaba ya Maaskofu wote, waumini na viongozi wengine wa Kanisa hilo kwa ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huu 2020.

Katika maelezo yake alimueleza historia ya Kanisa hilo ambalo lina Majimbo 71 hapa
nchini likiwemo Jimbo la Zanzibar na kueleza kuwa Kanisa hilo lilianza rasmi katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1927 na kuingia Zanzibar mwaka
1929 na mwaka 1939 lilipata usajili rasmi ambapo tayari limeshatimiza miaka 81.

Askofu Dk. Mtokambali alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuonesha ukaribu
mkubwa kwa madhehebu mbali mbali ya dini ya Kikristo wakati wa Kampeni na
kuzipongeza hotuba zake alizokuwa akizitoa ambazo zimewapa mwanga mkubwa
waumini hao na kusisitiza kuwa licha ya uchache wao lakini wamekuwa wakiishi salama
visiwani Zanzibar.

Kiongozi huyo pia, alipongeza uteuzi alioufanya Rais Dk. Mwinyi wa Mwakilishi wa
Baraza la Wawakilishi alietoka katika dini ya Kikristo Anna Athanas Paul ambaye
alisema anatoka katika kanisa la TAG.

Aidha, amesema kuwa Kanisa lao hilo lina Sera tatu ambapo ya kwanza ni ya kiroho, ya
pili ni kuendeleza utume wa kikristo na ya tatu ni kushiriki katika shughuli mbali
mbali za maendeleo ambapo kwa upande wa Zanzibar wameweza kushirikiana vyema
na Serikali zilizopita na kuahidi kushirikiana na Serikali hii ya Awamu ya Nane.

Amesema kuwa Kanisa hilo limekuwa likitoa msaada wa kuchimba visima, huduma za
elimu na za afya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo tayari kwa Zanzibar wana skuli
tatu za kiengereza na wanatarajia kujenga moja huko kisiwani Pemba.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Kanisa la TAG waliahidi kuendelea kushirikiana na
Rais Dk. Hussein Mwinyi pamoja na kuendelea kumuombea ili aendelee kuwa kiongozi
mwema na kuweza kuiongoza Zanzibar na watu wake pamoja na kuiletea maendeleo
endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here