Dk. Mwinyi afuata nyayo za JPM kubana matumizi

0

NA MWANDISHI WETU, DAR

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewaongoza Wazanzibari kusheherekea maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi huku akitoa sababu za kiuchumi na kubana matumizi ndiyo zimefanya shughuli hiyo kufanyika viwanja vya Mnazi Mmoja badala ya Amaan kama ilivyozoeleka.

Maadhimisho ya sherehe hizo zilizokuwa na shamrashamra aina yake zilifanyika jana katika viwanja hivyo na kuhudhuriwa na umati wa wananchi na viongozi wastaafu na viongozi waandamizi wa Serikali.

Miongoni waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah na marais wastaafu Dk Ali Mohamed Shein na Aman Abeid Karume.

Akieleza sababu ya kufanyia sherehe hizo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dk Mwinyi alisema “nilitamani kufanya sherehe za amsha amsha kama zilizopita. Lakini kwa vile kwangu ni mara yangu kwanza na hali ya uchumi  tulionayo tumelazimika kuadhimisha sherehe hizi kwa njia tofauti na mazoea yetu.

“Kama mnavyofahamu hali ya uchumi wa dunia imeyumba sana kutokana na madhara ya ugonjwa wa corona. Tumelazimika kupunguza baadhi ya shamrashamra ili fedha tutakazoziokoa zilielekezwe kufidia mapengo ya wajibu wa  Serikali,” alisema Mwinyi katika hotuba yake kwa Wazanzibari.

Dk Mwinyi ambaye amewahi kuwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), alisema “sina shaka hali hii ni ya mpito na siku za usoni ikitengemaa, tutarejea katika utaratibu wetu wa kawaida mapinduzi azim. Naamini mtatuelewa na kutuunga mkono,” alisema Dk Mwinyi.

MAFANIKIO NA MIPANGO

Akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nane alisema inaendelea kuchukua juhudi kubwa za kufufua uchumi wa visiwani humo.

“Hatua kwa hatua, hivi sasa, tunaendelea kushuhudia ongezeko la makusanyo. Kwa mfano, tayari makusanyo yemeanza kuongezeka kutoka bilioni 22 mwezi Oktoba hadi kufikia bilioni 36.9 mwezi wa Disemba, 2020 yaliyokusanywa na ZRB. Ni matuamini yetu kwamba hali hii itazidi kuimarika katika miezi inayofuata.

“Sekta ya utalii imeendelea kuimarika, ambapo tuliweka lengo la kupokea watalii 250,855 ifikapo Disemba 2020, baada kuzingatia mwenendo wa mardhi ya COVID 19 ndani na nje ya nchi yetu. Hadi Novemba 2020 jumla ya watalii 212,050 wametembelea Zanzibar sawa na asilimia 85 ya makadirio. Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta hii bado tunayo fursa ya kuindeleza.

“Hivi sasa, tunalitafutia ufumbuzi tatizo lililojitokeza la kuchelewa kupatiwa wageni huduma za msingi wanapofika katika Uwanja wa ndege na kuwasababishia usumbufu.

Kwa upande wa biashara alisema jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 62.2 zilisafirishwa kwenda nje ya nchi, Januari hadi Novemba mwaka 2020, ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 33.2 mwaka 2019 kwa kipindi kama hicho.

Kwa lengo la kuvutia wawekezaji alisema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara kuelekea eneo huru la uwekezaji la Micheweni, Pemba.

“Kadhalika, Serikali kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa au kuingizwa Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

“Napenda kukumbusha wananchi wenzangu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuendeleza sekta ya uchumi wa buluu ambayo ndio njia muhimu itayowezesha nchi yetu kupata maendeleo ya uchumi kwa kasi tunayoitaka.”

Alisema kupitia uchumi huo wa bahari unaofungamanisha sekta mbalimbali zikiwemo uvuvi, ufugaji wa kisasa wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki,ukulima wa mazao ya baharini, uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na sekta ya utalii. “Sekta zote hizo zitasaidia sana kutoa ajira za kudumu kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Aidha, uchumi wa buluu utachangia sana kuongeza mapato yatokanayo na kodi na ada mbali mbali.

Awali makamu wa pili wa rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah ambaye pia  mwenyekiti maandalizi ya maadhimisho hayo, alisema muonekano wa sherehe hizo mwaka huu ni kutoa fursa pia kwa wananchi kushiriki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here