Dk. Mwinyi aahidi ushirikiano na sekta binafsi

0
????????????????????????????????????

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itashirikiana vyema na sekta binafsi ili kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika zaidi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Ujumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), kufuatia muendelezo wa mkutano mkuu wa Wafanyabiashara wa Zanzibar, uliofanyika huko ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar mnamo Disemba 5, 2020.

Katika maelezo yake Dk. Mwinyi alisema kuwa azma yake ni kuimarisha  mashirikiano na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara.

Aliwataka kutoa ushauri juu ya Mamlaka za Udhibiti zipo nyingi ambazo zimekuwa zikileta mkanganyiko katika ulipaji wa kodi na kusisitiza haja ya Mamlaka hizo kuwa  pamoja na kuwa katika eneo moja ili kuondosha usumbufu.

Alisisitiza azma yake kwa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) katika kuhakikisha inajumuisha masuala yote muhimu kwa wawekezaji  ambapo wahusika wote ni lazima wawepo pamoja ili kurahisisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na utoaji wa vibali kwa wawekezaji.

Hivyo, Dk. Mwinyi alieleza haja ya sekta binafsi kutoa ushirikiano wake kwa kutoa ushauri ili kuhakikisha Mamlaka hiyo ya (ZIPA), inafanya kazi vyema katika kuwasaidia wawekezaji.

Alieleza haja ya kuwepo kwa mawasiliano kati ya sekta binafsi na Serikali kwa kujadiliana pamoja katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo na kueleza haja kwa Bodi hiyo kutafuta uwezo wa kuondoa matatizo katika sekta ya biashara kwa kupanga mambo vizuri.

Alieleza umuhimu kwa kufanyakazi kati ya sekta binafsi na sekta ya umma na kuwekwa watu wenye utaalamu katika kazi wanazozifanya.

Kwa upande wa uimarishaji wa viwanda vya ndani, Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuvilinda viwanda vya ndani ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ili kupatikana uwezo wa kuviendeleza na hatimae kuweza kuwasaidia wananchi wa Zanzibar hasa katika sekta ya ajira.

Aidha, Dk. Mwinyi alisisitiza haja katika kuwasaidia Wakandarasi wa Kizalendo ili kampuni zao ziweze kufanya kazi vyema hapa Zanzibar badala ya kuyatumia Makampuni kutoka nje hata kwa kazi ndogo hasa ikizingatiwa kwamba Wakandarasi Wakizalendo walio wengi Kampuni zao hazina uwezo mkubwa.

Alieleza umuhimu wa Vyuo Vikuu vyote kuweka mitaala inayohusiana na suala zima la ‘ Uchumi wa Buluu’, ili kuwepo kwa matayarisho ya kuelekea katika uchumi huo kama vile Sera zinavyoelezea kwani watendaji wakuu wa uchumi huo wanatarajiwa kutoka huko.

Halikadhalika Dk. Mwinyi alisema kuwa elimu ya kutosha inahitajika katika kuuelezea na kuufahamu ‘Uchumi wa Buluu’, hivyo muongozo unahitajika hasa kwa upande wa wanawake ili nao wajijue kuwa ni sehemu ya uchumi huo.

Alieleza azma yake ya kuanzisha utaratibu maalum wa kupokea changamoto kutoka kwa wananchi na hatimae changamoto hizo kupatiwa ufumbuzi kwa utaratibu maalum utaowekwa.

Dk. Mwinyi aliahidi kufanya mikutano na sekta zote za biashara na kuwataka wajiandae ili watakapokutana waweze kutoa changamoto zao ambapo Serikali kwa upande ake itaangalia namna ya kuzitafutia ufumbuzi hatua ambayo alisema ni nzuri kuliko kufanya kazi kwa makongamano na semina ambazo hazina tija.

Aliwasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi huku akisema kuwa kodi maalum zimewekwa Zanzibar ili kuwasaidia Wazanzibari kupata unafuu katika bidhaa zao licha ya kuwa bado wananchi wa kawaida hawanufaiki.

Kwa upande wa pili alisema kuwa kwa upande mwengine kodi kwa Zanzibar imeshushwa hivyo ni vyema viongozi hao wakawataka wafanyabiashara kulipa kodi kwani kodi hiyo ndio inayosaidia kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo elimu, afya na nyenginezo huku akiwataka wafanyabiashara kuwahurumia wananchi wa Zanzibar.

Aliwataka wafanyabiashara wazungumze juu ya kuwasaidia wanyonge sambamba na kufikia malengo katika kujenga nchi.

Alisema kuwa ipo haja ya kuangaliwa tena katika suala zima la mikataba kwani kuna baadhi ya mikataba serikali haipati mapato yanayostahiki.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here