Dk. Mwinyi aahidi kuongeza mishahara, posho

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo atapata ridhaa ya wananchi na kuwa rais, ataimarisha maslahi ya watumishi wa umma kwa kuongeza mishahara na posho kwa wakati.

Aliwataka wafanyakazi hao wa umma kuwa tayari kufanya kazi kwa bidii kwani wataboteshewa maslahi yao lakini watafanya kazi kwa kasi zaidi.

Ahadi hiyo aliitoa katika mwendelezo wa kampeni za CCM za kuwanadi wagombea wa CCM na kufafanua Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 huko katika kiwanja cha Dole Unguja.

Alisema mbali na kuimarisha maslahi ya makundi yote ya kijamii ikiwemo maslahi ya watumishi wa umma, pia atapitia upya maslahi ya wastaafu ili wapate pencheni kubwa kuliko wanayopata hivi sasa.

Aliwambia wananchi kuwa atalinda umoja wa kitaifa na kudhibiti vitendo vya ubaguzi wa kidini,kisiasa,kikabila.

“Nitadhibiti vitendo vya ukabila hapa kwetu kuna Upemba na Uunguja yote hayo nitayaondosha ili wote tuendelee kuwa wamoja”,alisema Dk.Hussein.

Dk.Hussein,alisema anaipongeza serikali ya awamu ya saba kwa hatua kubwa iliyopigwa katika sekta ya elimu kwa kujenga skuli za kisasa zenye vifaa vya masomo ya sayansi katika Mkoa huo

Alisema licha ya mafanikio hayo bado kuna changamoto za uchache wa madarasa na madawati mambo yanayotafutiwa ufumbuzi.

Alisema pia kuna upungufu wa walimu wa sayansi na masomo mengine chanfamoto itakayotafutiwa ufumbuzi.

Alisema serikali hiyo imejenga vituo vya afya vya kisasa vinavyotoa huduma bora kwa wananchi.

Alisema katika mkoa huo kuna vyanzo vingi vya maji safi na salama licha ya kuwepo na changamoto ya ubovu na uchakavu wa baadhi ya miundombinu na zitatafutiwa ufumbuzi.

Alitumia mkutano huo kujiombea kura na kuwaombea kura wagombea wote wa CCM aliwemo Dkt.John Pombe Magufuli.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alisema Zanzibar  imekuwa huru toka mwaka 1964 baada ya kufanyika mapinduzi ya mwaka 1964 na kwamba wananchi wanatakiwa kulinda tunu hiyo kwa kuichagua CCM.

Alisema mapinduzi hayo ni kielelezo tosha cha kulinda muungano na amani ya nchi.

Alisema mapinduzi hayo ndio msingi wa maendeleo ya nchi.

Alieleza kwamba baada ya mapinduzi serikali iliyoongozwa na rais wa kwanza marehemu Abeid Aman Karume,iliasisi mikakati ya maendeleo zikiwemo sera za elimu, bure,afya bure na kugawa ardhi bure kwa wananchi.

Katika maelezo yake Dk.Shein,alikemea vitendo vya kuwajeruhi wanachama wa CCM vinavyofanyika nchini katika maeneo mbalimbali na kuviita ni vitendo vya kihuni visivyofaa katika siasa za vyama vingi.

Alisema vyama vya siasa vishindane kwa sera na sio kuumizana kwani vitendo hivyo vinaweza kusababisha machafuko ya kisiasa.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni ya kiungwana wala haina malengo ya kuwaumiza wananchi badala yake itaendelea kufuata Katiba ya nchi na sheria ili kuendeleza amani iliyopo.

Aliwataka wananchi kuwa na amani na wajitokeze kwa wingi kupiga kura ifikapo octoba 28,mwaka huu kwani ulinzi umeimarishwa kila sehemu.

Pamoja na hayo Dk.Shein,aliwaombea kura wagombea wa wa Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi za Urais ,Ubunge,Uwakilishi na madiwani.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amesema CCM inalaani vikali vitendo vya uvunjifu amani vinavyofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa wapinzani vya kuwajeruhi wanachama wa chama hicho.

Dk.Mabodi, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki za kuthibiti vitendo hivyo visiendee na kwamba CCM haitolipiza kisasi bali itaendelea kudai amani mpaka wanashinda kwa kura nyingi na kuingia ikulu.

Alisema CCM imefanikiwa kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali katika kampeni zake kwa lengo la kueleza sera imara na kuwaomba kura ili waichague ifikapo octoba 28 ,mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here