Diwani wa CCM Hassan Shabani Mkata ajivunia mafanikio na maendeleo ya Kata yake Mungumaji Manispaa ya Singida

0
Diwani wa kata (CCM) ya Mungumaji na naibu meya manispaa ya Singida,Hassan Shaban Mkata,akichangia hoja kwenye kikao cha baraza la madiwani katika kipindi kilichopita.Picha na Nathaniel Limu.

Na Nathaniel Limu, SINGIDA

MBEGU utakayoipanda,ndiyo utakayoivuna.Hivyo ndivyo utakavyosema kuhusu mafanikio ya utendaji wa diwani mteule Mkata.

Katika nafasi ya udiwani,Mkata alipita bila kupingwa.Amesema utendaji na ukaribu wake kwa wapinga kura na wananchi kwa ujumla,vimembeba. Na vile vile kugofya wengine kuthubutu kugombea kata ya Mungumaji.

Kwenye udiwani hadi sasa amehudumu kwa miaka 15 (mara ya kwanza alianza ubunge 2005)

Mola akimjalia afya njema na nguvu,sasa anakwenda kuhudu kwa miaka mitano mingine.Akimaliza miaka hiyo mitano,atatimiza miaka 20 za udiwani.Ni madiwani wachache sana waliofikisha miaka hiyo.

Pia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,ameomba kurejesha nafasi yake nyingine ya unaibu meya.Ombi lake lilifanikiwa baada ya kuzoa kura 15 dhidi ya 11 za mpinzani wake pekee Geofrey Mdawa wa kata ya Mwaja.

Diwani mteule Mkata,ametoboa siri ya mafanikio yake yaliyopelekea kurejesha nafasi zake zote mbili,amesema pamoja na kubebwa na ukaribu wake kwa wapinga kura na wananchi kwa ujumla,ametekeleza ahadi zake binafsi karibu zote kwa wakati.Ahadi zilizotolewa kwenye ilani ya uchaguzi,nayo tumeitekeleza kwa kiwango kikubwa.Na siku zote amekuwa mkweli na muwazi.

Mkata mkulima na mfugaji maarufu,ametoa rai kwenye madiwani wenzake,kwaba nafasi hizi za uongozi ambazo ni dhamana,wajiepushe na vitendo vya kuvimba vichwa,kutokutekeleza ahadi binasi na ilani ya uchaguzi kwa wakati na kutokuwa wakweli na wawazi.

“Ukiacha vitendo hivyo na ukatekeleza kwa wakati ahadi zako binafsi na zile za ilani ya uchaguzi,utakuwa umeondoa/utapunguza maswali umiza wakati wa mikutano ya kampeni.Kwa kifupi nafasi yako ya kisiasa,utairejesha kwa urahisi mkubwa”,amesema.

Ameonya kwamba miaka mitano ni muda mfupi mno.Hivyo utekelezaji wa majukumu ya udiwani yanapashwa kuanzwa mara tu baada ya kuapa.Wale ambao wataona miaka mitano ni mingi,wanajidanganya.Utekelezaji wa ahadi tulizotoa,utekelezaji uanze mara moja.Wale watakaochelewa kuanza,itakula kwao.

MAFANIKIO

Diwani mteule mtoto wa tano katika familia yao, amesema katika kipindi hicho cha miaka 15 ya udiwani, kata hiyo imepata mafanikio ni mengi na makubwa ya kujivunia. lakini ametaja baadhi ambayo ni pamoja na ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata.

“Kabla sijaendelea, naomba nitumie fursa hii adimu kumshukuru Rais wetu Dk. Magufuli kwa utendaji wake uliotukuka. Zaidi kwa kitendo chake cha kutoa fedha za kutosha za miradi mbali mbali ikiwemo ya sekta ya elimu na afya katika manispaa ya Singida”,amesema.

Ameongeza kwa kusema serikali ya Magufuli imekuwa ikitoa fedha kwa wakati kitendo kilichochea miradi kukamilika kwa wakati, tofauti na huko nyuma.

Kuhusu ushiriki wa wananchi katika kutekeleza miradi yao,amesema wakazi wengi wamekuwa wakijitokeza kushiriki kujenga maboma ya shule za msingi na sekondari, serikali kuu imekuwa ikigharamia umalizaji wa majengo na kugharamia samani.

Diwani Mkata mwenye umri wa miaka 56 na siku 189,amesema changamoto ya wanafunzi kusoma nje ya Kata kwa sasa wameipatia ufumbuzi wa kudumu. Wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari,wanaenda shule na kurudi kula chakula cha mchana nyumbani kwao.Pia wamejenga shule shikizi.Kwa ujumla hakuna mwanafunzi ambaye anatembea umbali mrefu kwenda shule.

“Kama hiyo haitoshi, tumeanzisha sekondari ya kidato cha tano na sita.Matarajio yetu ni kwamba Kata yetu ya Mungumaji iwe ya wasomi wazuri wa kutosha.Kata ikiwa ya wasomi, kazi ya kilimo, kufuga, mafundi ujenzi, wafanyabiashara na wengine wa sekta mbalimbali, watafanya shughuli hizo kisomi. Kufanya kazi kimazoea, itabaki kuwa historia” amesema kwa kujiamini.

AFYA

Amesema kero ya miaka mingi ya kufuata huduma ya afya umbali mrefu, haipo tena. Baada ya Kata kushirikiana na Manispaa ya Singida kujenga zahanati yenye dawa na vifaa tiba vya kutosha.

“Kwa miaka mingi tumekuwa tukifuata matibabu hospitali ya Mkoa iliyopo Singida Mjini. Kufika katika hospitali hiyo kuna umbali mrefu, sio hivyo tu hospitali hiyo ina wateja wengi mno.Lakini sasa tunapata matibabu kwa mwendo mfupi. Zahanati ina dawa za kutosha akina mama wajawazaito wanapata huduma mchana na usiku”, amesema.

NISHATI YA UMEME

Diwani Mkata ambaye pia ni naibu meya manispaa ya Singida, amesema katika kipindi hicho cha miaka 15, Kata ya Mungumaji imefanikiwa kupata umeme wa mradi wa ‘Pre Urban’.

“Kwa sasa asilimia kubwa ya kaya katika Kata hiyo, zina huduma ya umeme. Kaya hizi zinautumia umeme huo kwa matumizi ya kijamii na za kiuchumi”,amesema.

Ameongeza kwamba baadhi ya wakazi wamefungua saluni zikiwemo za kunyoa, kuchomelea vyuma na majokovu ya kutunza juisi. Aidha,umeme huo unatumika kusukuma maji safi na salama. Taasisi zote zikiwemo shule za msingi na sekondari,zina huduma ya umeme” amesema.

Naibu meya huyo mteule,ametumia nafasi hiyo kulishukuru shirika la Tanesco kwa maamuzi yake ya kusambaza umeme katika vijiji vya Kata ya Mungumaji kwa gharama ndogo ya shilingi 27,000/= tu. Amesema mwananchi anaweza kuuza kuku wawili wa kienyeji, atalipia umeme na kubakiwa na chenji.

Aidha, amesema kupitia idara ya ardhi Manispaa ya Singida, kampuni ya binafsi inaendelea vizuri kupima viwanja katika Kata hiyo. Amesema viwanja hivyo ni vya makazi na taasisi mbalimbali. Jamii inashiriki kikamilifu kuhakikisha mradi huo unafikia malengo yake.

CHANGAMOTO

Diwani Mkata, amesema kwenye mafanikio yo yote hapakosi changamoto.

Hivyo ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na wananchi wachache na hasa vijana kugoma kuchangia mahitaji machache kwenye shule za msingi na sekondari.

“Serikali ya Dk Magufuli imeahidi kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne. Kweli tunashuhudia jinsi serikali kuu inavyotoa mamilioni ya fedha kugharamia masomo/elimu ya watoto wetu”,amesema na kuongeza;

“Lakini bado vipo changamoto ndogo ndogo ikiwemo ya chakula cha mchana kwa wanafunzi. Wazazi/walezi tunapaswa kuchangia elimu, ili watoto wetu waweze kusoma bila matatizo ya aina yo yote”.

Aidha,amesema kundi la vijana ndio pasua kichwa. Wakati wote wapo bize. Kundi hilo linahitaji kuelimishwa zaidi kwamba maendeleo ya kweli ya Kata yao, yataletwa na wao wenyewe wenye nguvu. Vijana wengi wanapotoshwa na vyama rafiki kwamba maedeleo ya kata yao ni jukumu la serikali. sio lao. Niwaombe vijana wabadilike na wasikubali kupotoshwa. Maendeleo ya Kata yao yanaletwa na vijana”, amesisitiza zaidi.

Ametaja changamoto zinginge kuwa jengo la utawala katika sekondari yao limejengwa mwaka 2008, lakini hadi sasa (2020) bado halijapauliwa. Shule ya msingi Mungumaji imefunguliwa mwaka 2006, hadi sasa bado haina nyumba za kusihi walimu. Jamii ilianzisha miradi hii ya shule ya msingi na sekondari inasubiri serikali kuu iwaunge mkono.

“Wananchi wengi wanatoa ushirikiano mkubwa sana katika kutekeleza miradi ya sekta mbalimbali. Lakini kuna wananchi wachache bado wana msimamo/mtazamo hasi.Hatutachoka tutaendelea kuwaelimisha kwamba wana jukumu la kushiriki kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kata ya Mungumaji”,amesema.

WITO KWA WAPIGA KURA NA WANANCHI KWA UJUMLA

Diwani mteule Mkata, pamoja na kuwashukru wapiga kura na wananchi wengine,amewaomba kila mmoja ajiulize ameifanyia nini Kata yake hasa katika kuiletea maendeleo. Vile vile wawe na subra na imani kwa serikali ya awamu ya tano ya Dk. Magufuli, ambayo inafanya mambo makubwa na mengi kwa kupindi kifupi sana.

UNAIBU MEYA MANISPAA YA SINGIDA

Amesema ametumikia nafasi hiyo nyeti kwa vipindi viwili tofauti. Kipindi hiki cha sasa na cha tatu.Amesema amesukumwa na demokrasia kuomba nafasi hiyo nyeti ambayo nayo ina changamoto zake,na wamewashukuru madiwani kwa kumwamini na kumrejesha tena katika nafasi ya unaibu meya.

“Lengo langu hasa ni kushirikiana na madiwani wenzangu kusogeza mbele maendeleo ya Kata 18 za Manispaa ya Singida. Na ushirikiano huo wa madiwani wote ambao ni wa CCM, utakuwa na nguvu zaidi kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yetu sote kwa ujumla”, amesisitiza

Naibu meya huyo mteule, ametaja baadhi ya miradi aliyoshiriki ni pamoja na ujenzi wa barabara nyingi za kiwango cha lami za Manispaa ya Singida.

“Kwa kushirikiana na Madiwani wote barabara nyingi za manispaa zina taa za barabarani na zile zinazoongoza vyombo vya moto. Tumejenga kituo kipya cha kisasa cha mabasi yaendayo mikoani. Mikoa mingi imefika kujifunza ujenzi wa kituo chetu cha mabasi. Hayo ni machache ambayo nimeshiriki kwa nafasi ya naibu meya”,amesema Mkata.

Aidha,naibu Meya huyo mteule, ametoa wito kwa wakazi wa manispaa ya Singida kuchapa kazi halali kwa bidii. Na washiriki kikamilifu kutekeleza miradi ya maendeleo, ili Manispaa hiyo ifike mahali, ipandishwe hadhi na kuwa jiji.

Aidha, amewataka wahakikishe wanajilinda na kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya Mapafu. Amesisitza zaidi kuwa gonjwa hilo hatari,lipo na linaendelea kusambaa sehemu mbalimbali duniani.

DIWANI NI NANI

Diwani ni mwakilishi, kiungo au nguzo kati ya wananchi na serikali ya Kata, wilaya na mkoa. Vile vile Diwani ana cheo cha mwenyekiti baraza la maendeleo (WDC) ya Kata. Ukiachilia mbali balozi wa nyumba 10, diwani yupo karibu zaidi na wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here