COSTECH inavyowaibua Waandishi wa habari kwenye Ufugaji

0

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

ILIKUWA Desemba 15-16 Mwaka 2020 ambapo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)iliendesha mafunzo ya uandishi wa habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kwa wanahabari 25 wa mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu namna ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za kisayansi na ubunifu kwa jamii kupitia tafiti mbalimbali .

Mafunzo haya yalifanyika kwa siku mbili mfululizo jijini Dodoma ambapo yalihusisha jumla ya washiriki 40 kwa mchanganuo wa wanahabari 25 na watafiti 15 na baadaye Tarehe17-18 kuendelea na ziara ya mafunzo kwa kutembelea vituo vya utafiti na ubunifu ili kupata vyanzo vya habari

Jambo hili lilionekana jepesi na lilichukuliwa ki kawaida sana kwa baadhi ya wanahabari hasa kutokana na wengi wao kutokuwa na ndoto za kuwa wakulima au wafugaji.

Hii ni kutokana na wanahabari wengi kuwa na mazoea ya “upendo wa mshumaa”, kumulikia wenzake, hata katika kumulika huko, wenyewe unateketea!

Tofauti na ilivyozoeleka, baadhi ya wanahabari suala hili wamechukuliwa kama fursa ya kujiendeleza kupitia mafunzo hayo kwani mbali na kufanya kazi iliyokusudiwa na Tume kuhusu namna bora ya kuipasha jamii kususu tafiti mbalimbali za masuala ya kilimo na ufugaji kwa lugha nyepesi,baadhi ya wanahabari wamejikuta wakishawishika kuingia moja kwa moja katika ufugaji wa kisasa .

Saleh Ramadhan ni mmoja wa wanahabari waliopatiwa mafunzo hayo na kujikuta anashawishika kujiingiza kwenye Ufugaji wa kuku chotara kutokana na umuhimu wake katika kukabiliana na wimbi la umasikini kwa kuongeza kipato cha familia yake.

Anazungumzia ufugaji wa kuku kuwa na faida kubwa kutokana na soko la uhakika hasa ukizingatia Jiji la Dodoma kuwa na muingiliano mkubwa wa watu hivyo kumwezesha ipasavyo kupambana na umaskini .

“Ni mazoea kwa jamii nyingi Tanzania kufuga kuku kama sehemu ya mila na desturi zao,Kuku amekuwa akifugwa bila kupatiwa huduma muhimu kama makaazi bora, chakula cha ziada, tiba, kinga za magonjwa mbali mbali jambo hili linawatatiza baadhi ya wafugaji ,”anasema Ramadhan.
Kwa kuanza ufugaji ameanza na kuku 100 ambapo amezingatia maelekezo ya madaktari wa mifugo kutoka Taasisi za utafiti ambao walimshauri kuwa,ili apate kundi lenye kuku bora hana budi achague jogoo bora na matetea bora.

Kwa maana hiyo alianza na uchaguzi wa aina ya kuku bora ambao ni chotara yaani mchanganyingo wa aina mbili za kuku, Mfano kuku mchanganyiko wa kienyeji na kuku wengine wa kigeni.

“Wakati wa uchaguzi wa mbegu nilizingatia jogoo wenye umbo kubwa wanaokua haraka na wenye uwezo wa kustahimili magonjwa ikiwa ni pamoja na matetea wanaoweza kutaga mayai mengi,Jogoo ninaowachagua kwa ajili ya matetea au makoo yao wasiwe na uhusiano wa damu,”anaeleza

Ukiishachagua wazazi wa kundi lako changanya jogoo na matetea kwa uwiano wa jogoo mmoja kwa matetea 10 . Ukiwa na matetea 20 utahitaji kuwa na jogoo wawili.

Anaeleza sababu za kuchagua kufuga kuku chotara kuwa wanastahimili magonjwa,Wanataga mayai mengi mpaka 240 kwa mwaka kama ukiwalisha vizuri .

“Nimeshawishika kwa kuwa Wanafikisha mpaka kilo 3 kwa muda wa miezi mitatu kama ukiwalisha vizuri,hutumika kama kuku wa nyama na mayai na kwamba Ukitaka kufuga kuku kibiashara usimwachie kuku kuatamia mayai kwani unampotezea muda wa kutaga.

“Ukitaka kupata faida kubwa usinunue chakula bali tengeneza
mwenyewa kwani bei za vyakula zimepanda sana, kwenye ufugaji asilimia 80 inaenda kwenye ulishaji na asilimia 20 inaenda kwenye madawa.

Hata hivyo anaeleza kuwa ili kuku wawe na afya nzuri ,Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari.
“Nilifanya uchaguzi mzuri wa fundi ambaye ametengeneza banda hili lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga”anafafanua.

Aidha anatoa angalizo kwa watu naotamani kufuga kuku kuzingatia kutumia vifaa na vyombo maalum ili kurahisisha na kuboresha utunzaji wa makundi mbalimbali ya kuku.

“Vifaa na vyombo vinavyohitajika kwa ajili ya kuwekea chakula na maji, kutagia mayai na kupumzika vinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za mifugo wakati mwingine natengeneza mwenyewe kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye mazingira yangu,’’anasema.

Hiyo ni hamasa ambayo mwanahabari huyo ameipata kutokana na mafunzo kwa njia ya vitendo yaliyofadhiliwa na COSTECH.

Hata hivyo anakiri kuwa huo sio mwisho wa kujifunza masuala ya ufugaji na kwamba ataelekeza zaidi nguvu katika kujifunza ufugaji wa kisasa hadi kufikia malengo aliyojiwekea ya kuwa wa kimataifa kwa kuanza kusafirisha kuku wa nyama nchi ya nchi.

Kutokana na hayo,mtaalamu wa masuala ya mifugo ambaye ni Mtafiti mwandamizi wa mifugo kutoka Taasisi ya utafiti wa mifugo Tanzania (TARILI) Kituo cha Mpwapwa Mary Mwangoka anaeleza kuwa wafugaji wanapaswa kuwakinga kuku na maradhi.

Mwangoka anasema,kuku wanaopata lishe bora, kutunzwa vizuri na kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa yanayotokea huwa na afya nzuri.

“Ni bora kuzuia magonjwa kuliko kutibu ili kupunguza vifo na gharama,iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa watenganishwe na kuku wasio wagonjwa na wapatiwe tiba”anasema Mtaalamu huyo.

Licha ya hayo anaeleza kanuni muhimu za kufuata ili kuzuia magonjwa kwamba kabla ya kuweka kuku, banda linyunyuziwe dawa ya kuua wadau wa magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwakagua Kuku kila siku ili kubaini wagonjwa au wenye matatizo, kuwatenga na kutoa taarifa kwa mtaalam wa mifugo,
ili wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali,”anasisitiza.

“Watu wasiohusika wasiingie eneo la kufugia kuku bila utaratibu,
Ndege na wanyama wengine wasifike eneo la kufugia kuku,banda la kufugia kuku litenganishwe na mabanda ya mifugo mingine na lango la kuingia katika banda la kuku liwekewe dawa ya kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea vya wadudu wa magonjwa na
Vifaa vya chakula na maji viwe safi wakati wote”anasema Mwangoka.

Aidha anaeleza kuwa Magonjwa ndio husababisha hasara katika mfumo wa ufugaji wa kuku na kwamba kinga yaweza kutolewa mara kwa mara (kila baada ya miezi mitatu) dhidi ya magonjwa.

Anasema “Siku 2-6 Pullorum Trisulmycine, Trimazine 30% au Cotrim+Vitalyte, Amin’total au Broiler booster,Siku ya 7 Mdondo(newcastle) Newcastle vaccine(Lasota,Siku 14 Gumboro Gumboro (Bursine vaccine-IBD) ,Siku 16-20 Coccidiosis Trisulmycine/Trimazine/Esb3 30%+Dawa yoyote ya Vitamin ya maji,Siku 21 mdondo(newcastle) Newcastle vaccine(Lasota) maji,Siku 28 Gumboro Gumboro (Bursine vaccine-IBD) ,”anafafanua na kuongeza;

Wiki ya 6-8 Ndui Fowl pox vaccine sindano,Wiki ya 13 minyoo Pipperazine cirtrate+ Dawa yoyote ya vitamin Wiki ya 10 hadi ya 15 ukataji midomo Dawa ya vitamin itumike”anasema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here