China yasema iko tayari kununua samaki kutoka Tanzania

0

   >> Asisitiza  soko la samaki  nchini humo ni kubwa

Na  AZIZA MASOUD,DAR ES SALAAM

SAMAKI ni moja ya biashara kubwa ambayo inafanywa na watanzania wengi na kujipatia kipato,wapo  wanaofanya biashara hiyo kama wachuuzi wadogo wadogo na pia wapo wanaouza nje ya nchi.

Biashara ya samaki kwenda nje ya nchi inaonekana kukua siku hadi ambapo  mapema mwaka jana mawaziri wa wizara tatu,makatibu wakuu pamoja na wakuu wa Mikoa ya Mwanza,Kagera na Mara walikutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja ilikuhakikisha biashara ya minofu ya samaki katika masoko ya nje ya nchi inakuwa endelevu

Lengo la kikao hicho  ilikuwa ni kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha biashara iliyoanza Mei 12 mwaka jana   ya kusafirisha samaki kwenye masoko ya nje kutokea uwanja wa ndege wa Mwanza ikuwa endelevu.

Mpango huo umeanzishwa ili  kuwezesha kukuza uchumi wa wananchi wa Kanda ya Ziwa  pamoja na taifa kwa ujumla,watakao pata faida moja kwa moja katika mnyororo  huo wa biashara ni wazalishaji wa samaki pamoja na taasisi ambazo zitakusanya tozo kutokana na huduma zitakazotolewa.

Taasisi zinazonufaika na mpango huo  ni pamoja na Mamlaka ya  ya viwanja vya ndege,mamlaka ya Udhibiti usafiri wa anga na Mamlaka ya hali ya hewa ambapo pale itakapowezekana  waongeze aina zingine za bidhaa au mazao yanayoweza kusafirishwa kwenda masoko ya nje ya nchi ili kuongeza wigo wa wanufaika kama vile wanavyojua kuwa ukanda huu ni wa mifugo ikiwemo ng’ombe na  mbuzi.

Wakati mpango huo ukiendelea wiki hii imejtokeza fursa nyingine kwa wafanyabiashara hao wa samaki nchini ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa China,Wang Yi amesema kuwa nchi yake inakaribisha    samaki kutoka Tanzania kuuzwa moja kwa moja nchini humo ili kusaidia sekta ya   maendeleo  ya uvuvi nchini.

Akizungumza mwanzoni mwa wiki hii  wakati alipotembelea Mwalo wa Chato beach uliopo katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, na kukutana na wavuvi  Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa China amesema kuwa  soko la samaki China ni kubwa na hivyo anakaribisha samaki kutoka Tanzania kuuzwa nchini kwake.


“Nimeambiwa wakati wa mvua Tanzania hali inakuwa ngumu sana na soko la samaki huko China ni kubwa. Kwa hiyo ningependa kutangaza kwamba China inakaribisha samaki kutoka Tanzania na pia tungependa kuwasaidia kuongeza mapato na kuboresha maisha yenu”.

Amesisitiza “Tunapenda kusaidia kuuza bei ya samaki watanzania kupitia mkataba husika ili mazao kutoka Ziwa Victoria yaende China kwa urahisi zaidi.”

Vilevile, Waziri Wang  amesema kuwa   Ubalozi wa China nchini  utatoa  kiasi cha dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kusaidia wavuvi wa mwalo wa Chato kununua vifaa vya uvuvi.

Aidha, alionesha kufurahishwa  na  zawadi ya samaki aliyopewa na wavuvui wa mwalo huo .

“ Leo nyinyi mmenizawadia samaki wazuri na wakubwa sana,  nimefurahi sana na nashukuru sana, kitendo  hili  kinaonesha  hisia zenu na urafiki wa kweli.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashamba Ndaki amesema  kuwa Tanzania imejaliwa rasilimali za uvuvi katika maeneo mbalimbali ya maziwa, mito na  bahari ambazo zinachangia pato  la taifa, ambapo asilimia 75 ya mazoa ya uvuvi yanayozalishwa hapa nchini yanavunwa kutoka Ziwa Victoria.

Waziri Ndaki alitaja mazao hayo matatu ya kibiashara kuwa ni samaki aina ya sangara, sato na dagaa.

“Mazao yatokanayo na samaki aina sangara yanayojumuisha minofu na mabondo ndio husafirishwa kwa wingi kwenda kwenye soko la kimataifa ikiwemo China, kwa kupitia Hong Kong. Ni lengo la serikali yetu kuuza zao hili moja kwa moja nchini China.”amesema Waziri Ndaki

Amefafanua kuwa matarajia ya Serikali ni kusaini  mkataba utakaowezesha kuuza bidhaa hizo moja kwa moja katika soko la China.

“Tunaomba mheshimiwa  Waziri Wang mara tutakapowasilisha rasmi maombi ya soko la mabondo tuungwe mkono na Serikali ya China. Tuna imani kwamba kufunguliwa kwa soko hilo kutasaidia sana jitihada za wananchi kujikwamua na umasikini” amesisitiza Waziri Ndaki.

Tanzania ina mialo 1,373 ikiwamo mwalo wa Chato licha ya Serikali kufanya  juhudi za kuendelea mialo hiyo hapa nchini bado kuna fursa ya kuboresha miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kuchakata mazao ya samaki.

Aidha, Waziri Ndaki ameiomba Serikali ya China kuhamasisha makampuni binafasi kutoka nchini humo kuja kuwekeza katika viwanda na miundombinu ya vuvuvi ili kuongeza uzalishaji kupunguza upotevu wa rasilimali za uvuvi na kuongeza ubora na usalama wa mazao ya uvuvi hapa nchini.

 “Zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanajishughulisha na shughuli mbalimbali katika mialo, na sekta ya uvuvi inawapatia kipato na lishe wananchi na kuchangia pato la taifa.”amesema Waziri Ndaki

Asilimia 85 ya mazao ya uvuvi yakiwamo yale yanayosafirishwa nje ya nchi yanatokana na wavuvi wadogo wadogo ambao hutumia vyombo vidogo vya kuanzia mita tatu hadi mita 10.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wavuvi katika mwalo wa Chato Beach, Kamese Kalima alisema mwalo  huo umeanzishwa mwaka 1999  ukiwa na wavuvi 500 na mitumbwi 125, na kati ya hiyo mitumbwi 110 ni ya makasia na mitumbwi 15 ni ya injini.

Kalima aliiomba Serikali ya China kuwasaidia kutatua changamoto za miundombinu  zinazowakabili ambazo ni vyombo vya uvuvi, jengo ambalo litajumuisha soko la uvuvi, mitambo ya kuzalisha tani 5 za barafu, chumba cha ubaridi chenye uwezo wa kuhifadhi tani 10 za samaki, na mashine ya umeme yenye uwezo wa kukaushia tani 5 za dagaa kwa siku.

 “Tunatambu China ni vinara wa viwanda vya samaki duniani, hivyo tunaomba miundombinu ya uchakataji samaki na China kuja kuwekeza viwanda vya kuchakata samaki angalau tani 35 kwa siku.” Amesema  Kalima

Mwalo wa Chato na Mkoa wa Geita kwa ujumla unazalisha zaidi ya tani 23,844  za samaki kwa mwaka ambao husafirishwa umbali mrefu kwenda viwanda vilivyopo Kagera na Mwanza kwa ajili ya kuchakata samaki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here