Chalamila: Ni aibu na fedheha utoroshaji madini mbeya

0

Sakata la utoroshaji dhahabu lililowahusisha askari polisi wawili na wafanyabishara watatu wa madini wilayani Chunya limeingia katika sura mpya baada ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kusema ni aibu na fedhea kwa viongozi wa mkoa.

Chalamila amesema hayo leo Desemba 14, mbele ya Waziri wa Madini, Dotto Biteko kwenye mkutano wa wachimbaji wadogo wa dhahabu na wadau wa madini wilayani Chunya.

Chalamila amesema utoroshaji huo wa madini umewadhalilisha viongozi na walipaswa kujipeleka polisi ili wahukumiwe walau miezi sita jela.

“Kimsingi, mkoa na viongozi tumedhalilika sana. Tulipaswa kujipeleka wenyewe polisi na si vinginevyo,” amesema.

Mwenyekiti wa wachimbaji madini Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha amesema changamoto nyingine inayosababisha utoroshaji wa dhahabu ni utoaji holela wa leseni hivyo ni vyema mifumo hiyo idhibitiwe na ufanyike utafiti wa kina katika maeneo ya migodi wilayani humo.

Amesema kumekuwa na tabia kwa mchimbaji mmoja kuwa na vibali vitatu mpaka vinne hivyo kuwa sababu ya wizi na utoroshaji dhahabu.

Kwa upande wake, Waziri Biteko amesema Tanzania ina wachimbaji wadogo zaidi ya milioni sita wanaofikiwa kupitia vyama vyao.

“Tumefuta leseni nyingi za wachimbaji wakubwa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata leseni kupitia vyama vyao na kutaka uongozi wa mkoa kusimamia hili,” amesema Biteko

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here