Chadema, ACT-Wazalendo waumbuka

0

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

JANA imedhihirika wazi kuwa ushindi wa kishindo wa Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu, umetokana na maamuzi ya wananchi wengi baada ya vyama vinavyopinga uchaguzi huo kuambulia patupu katika mpango wao wa kutaka wananchi waandamane.

Viongozi wa Chadema na ACT-Wazalendo walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita walikutana na kupanga kuanza maandamano kuanzia jana nchi nzima wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupinga uchaguzi huo ambao wananchi waliichagua CCM kwa kishindo.

Hata hivyo wananchi wamepuuza wito huo na kusema kuwa hawawezi kupinga uchaguzi ambao wengi wameshinda kihalali katika uchaguzi huru na wa haki na katika mazingira ya amani.

Walisema Chadema ambao wamekuwa wakilia na demokrasia wenyewe wameshindwa kuheshimu maamuzi ya walio wengi kwa kukataa matokeo ya uchaguzi ambao kila mtu maeshuhudia ulivyokuwa wa amani, huru na haki.

“Unaposema unadai demokrasia halafu wewe mwenyewe hukubaliani na mifumo ya kidemokrasia kama uchaguzi huru na haki,” alisema Abdallah Kassim mkazi wa Buguruni eneo ambalo ndipo vyama hivyo vilipanga kuanza maandamano.

“Wenyewe wamejiumbua kwani kutojitokeza kwa watu kuwaunga mkono, inamaanisha watu wengi waliichagua CCM ndo maana hawawezi kupingana na kile walichokichagua wameendelea na shughuli zao,” aliongeza.

Eusebius Kajuna mkazi wa Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam alisema anakubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu ambayo CCM imeibuka kidedea na kusema hilo limetokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya awamu ya Tano na wananchi wamerudisha shukrani kwa kuipa ushindi wa kishindo.

“Ingekuwa kweli wananchi hawajaichagua CCM basi kila mtu angetoka barabarani kupinga uchaguzi lakini kilichopo ni wachache ambao wameshindwa kwenye uchaguzi wanataka ajenda yao iwe ni ajenda ya umma lakini naamini leo wataelewa kuwa wananchi ndo wameamua kuipa CCM ushindi wa kishindo,” alisema Kajuna.

Esther Michael mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam alisema Chadema kutokukubali matokeo ya uchaguzi ni kupingana na nguvu ya umma ambao umeamua kuichagua CCM.

“Wanaimba wimbo wa demokrasia lakini wenyewe wameshindwa kuucheza kwasababu kama unapinga uchaguzi basi wewe umeshindwa kuheshimu demokrasia na maamuzi ya wengi maana demokrasia ni wengi wape, sasa wao wachache wamekosa halafu wanataka wale wengi ndo wapingwe ? wameshindwa kwenye maandamano yao maana hayajaanzia kwa watu bali ni kundi lililokosa kuchaguliwa ndo wanapinga,” alisema Esther.

Baadhi ya viongozi wa upinzani nchini Tanzania wanashikiliwa na polisi baada ya kutangaza kupanga maandamano hayo yaliyofeli.

Polisi walisema wamemkamata mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chadema ,  Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam Boniface Jacob.

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa alisema walipiga marufuku maandamano hayo yaliyopangwa kuanza jana asubuhi, lakini viongozi wa Chadema “wameonekana kufanya vikao kuratibu maandamano ya fujo”.

Alisema viongozi hayo walipanga kuhatarisha usalama wa raia kwa kwa kufanya vurugu kuonyesha kutokubaliana na matokeo, watu hao wanapanga kuingia mtaani kuchoma maeneo mbalimbali kama masoko, magari na vituo vya mafuta.

Aidha alisisitiza kuwa operesheni kubwa inaendelea kwa yeyote ambaye atashiriki kuratibu, kuwezesha au kushiriki katika maandamano hayo atafikishwa kwenye mikono ya sheria.

BODABOBA SINGIDA WAPINGA

Dereva wa Bodaboda Manispaa ya Singida, Ramadhani Zuberi akitoka ufafanuzi kwa waandishi ambao hawapo pichani kupinga na kulaani maandamano ya vijana ambao wanataka kutumika kuvuruga amani.

Wamiliki na Madereva wote wa Bajaji Mkoa wa Singida wametoa tamko rasmi la kulaani baadhi ya vijana ambao wameanza kutumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani kuandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, Mwaka huu.

Akitoa  tamko  kwa  niaba ya  wanachama 2000 wa  Mkoa wa Singida  kwenye Kituo cha Bajaji  Soko Kuu la Mjini Singida, Mwenyekiti wa Madereva na Wamiliki wa Bajaji na Boda boda  Manispaa ya Singida, Ahmed Juma alisema  umoja wao  umepinga njama  zinazofanywa  na  baadhi ya  vyama  ya kuwatumia madereva  hao na kusisitiza kuwa njama hizo hazitafanikiwa katika Mkoa  wa Singida .

“Tumejipanga kukabiliana na uhuni wowote ambao umepangwa kufanywa kwenye kipindi  hiki na baadhi ya wahuni wachache wasioitakia mema  nchi yetu, tunaomba  vyombo  vya ulinzi visimamie hili kikamilifu na sisi tupo nyuma yao” aliongeza Juma.

Alisema kinachotaka kufanyika sasa baada ya  uchaguzi kukamilika na matokeo  kutangazwa  kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi na Mamlaka halali ni  vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo amesema halikubaliki badala  yake amewasihi wananchi wafanye kazi  ili  kuiletea nchi yetu maendeleo  zaidi katika awamu ya sasa.

Aliumwomba Rais, John Magufuli  kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania ili itoke kwenye Uchumi wa Kati  hadi Uchumi wa juu kabisa  na hatimaye  kuboresha maisha  ya watanzania wote.

Mwenyekiti wa Madereva wa Boda boda  wa  eneo  la Soko Kuu Mjini Singida, Kulwa Moshi  alionya madereva wa  Bodaboda ambao kwa namna moja au nyingine  watatumika katika kuvunja Sheria za nchi kwa kupanga  njama za kufanya maandamano  yasiyo ya amani.

Moshi aliongeza kuwa wananchi wameamua kuwachagua viongozi wanao wapenda hivyo hakuna sababu ya watu kuandaa njama za kupinga matokeo ya uchaguzi.

Naye Ramadhani  Zuberi,  Dereva wa  Bajaji kwenye  Kituo Kikuu cha Mabasi  ya Mkoa wa Singida alipongeza Serikali kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kwa uwazi  ambao umeweza kufuata taratibu zote na kutoa matokoa kwa wakati

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC), Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5 Mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here