CCM Zanzibar wapongeza hotuba ya Dk. Mwinyi

0

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimepongeza hotuba iliyotolewawa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,kuwa imetafsiri muelekeo halisi wa maendeleo endelevu ya nchi chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nane ya Zanzibar.

Hotuba hiyo ilitolewa juzi na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, wakati akizindua Baraza la 10 mkutano wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani nje kidogo ya Zanzibar.

Imebainisha, hotuba hiyo licha ya kufafanua kwa kina namna serikali itakavyopaisha uchumi wa nchi, pia imezingatia maslahi ya makundi yote ya kijamii.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar  Catherine Peter Nao, akiwa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Alisema, Rais ameahidi kuijenga Zanzibar mpya kupitia uchumi wa kisasa wa buluu (blue Economy) unaopatikana kupitia rasilimali ya bahari.

“Kupitia uchumi wa bahari unaofungamanisha sekta mbalimbali zikiwemo uvuvi, ufugaji wa kisasa wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki, ukulima wa mazao ya baharini ikiwemo mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na sekta ya utalii zote hizo zitatoa ajira za kudumu kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema Catherine na kusisitiza:

CCM Zanzibar inampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hotuba yake iliyoonyesha dhamira,dira,mipango endelevu na malengo halisi ya Serikali ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar bila ubaguzi wa rangi,kabila na itikadi za kisiasa kwani maendeleo hayana chama.

Alisema, CCM imekuwa ni chama cha kisiasa cha kwanza nchini Tanzania tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992, kilichoeleza kupitia miongozo ya Kikanuni, Kikatiba na machapisho yake mbalimbali kuwa kinachukia vitendo vya rushwa na ufisadi jambo ambalo Rais Dk. Mwinyi ameahidi kudhibiti vitendo hivyo vinavyokwamisha maendeleo. 

Aidha, alibainisha kuwa CCM inawataka viongozi na watendaji mbalimbali waliopewa dhama za uongozi kutekeleza wajibu kwa kasi na matarajio ya Rais Dk.Hussein ili wananchi waliowachagua kwa kura nyingi waendelee kukiamini Chama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here