Bunge la 12 kuanza Novemba 10 Dodoma

0

Na Dotto Kwilasa, Dodoma 

KATIBU  wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania Steven Kagaigai ametangaza kuanza kwa Bunge la 12 Novemba 10 mwaka huu jijini Dodoma.

Aidha amewataka  wabunge wa kuchaguliwa na kuteuliwa kufika katika ofisi za Bunge wakiwa na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kujisajili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Kagaigai alisema usajili wa wabunge umeanza Jana katika ofisi za Bunge hilo hadi Novemba 9.

“Usajili unaanza leo Novemba 7 hadi 9 mwaka huu katika ofisi za Bunge jijini Dodoma ambapo wabunge wanatakiwa kufika na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya usajili,”alisema.

Katibu huyo wa Bunge alizitaja nyaraka hizo kuwa ni pamoja na Hati ya kuchaguliwa au kuteuliwa,nakala ya kitambulisho cha NIDA ,Kadi ya benki ya Mbunge  na cheti  cha ndoa kinachotambuliwa na serikali.

Nyaraka  nyingine  ni vyeti vya kuzaliwa vya watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ,vyeti vya elimu ya Mbunge ambavyo husaidia namna ya kuwapanga wabunge katika kamati za Bunge pamoja na picha ndogo (passport size) nane.

Kwa upande wa Wabunge wa kuteuliwa Kigaigai alisema wanatakiwa kwenda na Hati ya kuteuliwa kuwa mbunge, Nakala ya kitambulisho cha Taifa, kadi ya benki yenye jina la mbunge, cheti cha ndoa kinachotambuliwa na serikali kwa wenye ndoa, cheti cha kuzaliwa cha watoto wenye umri chini ya miaka 18, vyeti vya elimu, nakala ya wasifu wa mbunge na picha nakala tatu.

Kagaigai alisema shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kusomwa kwa tangazo la Rais la kuitisha bunge,uchaguzi wa spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitisha jina la waziri mkuu na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuanza kwa Bunge kunafuatia tangazo la Rais la kuitisha Bunge lililotangazwwa kwenye gazeti la Serikali Toleo maalum la Novemba 5, 2020 na kufuatia tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali Toleo maalum la kutangaza nafasi ya Spika kuwa wazi na utaratibu utakaotumika kujaza nafasi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here