Bobi Wine afuata nyayo za Kizza Besigye

0
Na Mwandishi Wetu

Aliyekuwa rais wa Tanzania awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema kila zama na kitabu chake, akimaanisha haiba au mtindo wa uongozi na siasa za nchi katika kipindi fulani ipo tofauti baina ya mtawala mmoja na mwingine.

Katika siasa za upinzani zipo zama tofauti baina ya haiba na mtindo wa mwanasiasa fulani au vyama vya siasa kulingana na mazingira waliyomo.

Hivi ndivyo zilivyo tofauti kati ya Chama cha Forum for Democratic Change (FDC) cha Kizza Besigye na National Unit Platform (NUP) cha Robert Kyagulanyi ambaye lakabu yake ni Bobi Wine.

Kwa NRM ya Museveni muundo wake umejengwa katika msingi wa kivita yaani kupigania ukombozi na madaraka nchini Uganda kabla ya kuwa chama cha siasa, wakati FDC ni zao la siasa za harakati kama kilivyo chama cha NUP.

Haiba ya Kizza Besigye imejikita katika hekaheka za siasa za upinzani mbali ya kuwa tabibu akiwa amegombea urais mara nne.

Wakati Robert Kyagulanyi amejenga haiba yake kupitia muziki kabla ya kuingia siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Kyadondo mashariki amebeba matumaini ya watu katika siasa za upinzani.

Historia ya siasa za Uganda haijawahi kuona viongozi wakakabidhiana madaraka kwa amani.

Museveni aliingia madarakani baada ya vita vya msituni na kumng’oa rais Tito Okello.

Je nini kinachopaswa kuzingatiwa kwa wanasiasa hawa wawili, Kizza Besigye na Bobi Wine?

Vyombo vya dola vimekuwa vikitumia kila mwanya kumnyamazisha mwanasiasa huyo kwa nyakati tofauti.

Bobi Wine kati ya wanasiasa ambao wamekutana na rungu la dola, kukamatwa mara kwa mara kwa madai mbalimbali, kusota rumande, kupigwa na kuumizwa hadi kukimbilia nchini Marekani kupata matibabu.

Kufunguliwa kesi za kisiasa, kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara maeneo, wafuasi wake kupigwa mabomu ya machozi na kuvurugwa kisaikolojia kwenye mipango yake ya kisiasa.

Hayo ndiyo maisha aliyoishi mwanasiasa mkongwe Kizza Besigye.

Ingawa amestaafu siasa za majukwaani lakini ameacha alama muhimu kambi ya upinzani akiwa mgombea ambaye amemtetemesha mara nyingi Museveni kupitia chaguzi za mwaka 2001, 2006, 2011 na 2016.

Mchakato wa karne mbili

Tofauti ya kisiasa Bobi Wine na Kizza Besigye ni vizazi vya karne mbili tofauti.

Bobi Wine anatumia kizazi kipya, ambacho idadi kubwa ya wananchi wake ni vijana waliozaliwa katika karne ya 21 na wachache waliozaliwa mwishoni mwa karne ya 20.

Vijana waliozaliwa mwanzoni mwa miaka 2000 maana yake sasa wana miaka 20, ambalo ni kundi kubwa kwenye uchaguzi huu.

Wakati Kizza alikuwa alitegemea kizazi kilichozaliwa wakati wa karne ya 20 na kizazi kilichokulia karne ya 21.

Tofauti hii inampa mwanya Bobi Wine kupata uungwaji mkono kwa wingi kutoka kizazi kipya.

Kwanza ameungwa mkono katika kazi yake ya muziki na upande wa pili ni kuingia siasa maana yake amehamisha mashabiki waliomhusudu kwenye muziki na kuongeza wengine wanaompenda kama mwanasiasa.

Harambee kutoka Ulaya hadi Uganda
Harambee ni miongoni mwa mambo muhimu katika kampeni za uchaguzi mkuu.

Wanachama, wafuasi, marafiki na wadau wa siasa wanaweza kumchangia fedha za kampeni mgombea wanayemtaka.

Kizza Besigye alikuwa mahiri katika eneo hili, lakini kampeni za Bobi Wine, ambaye amekuwa akiandika mara kwa mara katika mitandao ya kijamii na kuzitaja nchi na wakusanyaji wa michango ya fedha kutoka kwa mamia ya raia wa Uganda wanaoishi nchi mbalimbali barani Ulaya, Marekani, na Asia.

Nguvu na ushawishi wake katika siasa

Uchaguzi wa mwaka 2016 vyama vya upinzani vilishindwa kuelewana, lakini kambi hiyo ilibakiwa na wanasiasa wenye nguvu.

Kizza Besige aligombea kupitia chama chake, huku akimwachia Amama Mbabazi (waziri mkuu wa zamani) kuunda muungano mdogo wa upinzani.

Hata hivyo muungano ulioundwa na Mbabazi ulikosa nguvu na ushawishi wa Besigye ambaye matokeo ya uchaguzi yameonesha akishikilia nafasi ya pili nyuma ya Museveni.

Kambi ya upinzani katika uchaguzi wa 2021 haina nguvu za Besigye, badala yake Bobi Wine ndiye ameibuka kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa miongoni mwa wapiga kura na wafuasi wa kambi hiyo.

Kustaafu kwa Besigye kunamnufaisha Bobi Wine na huenda akafanikiwa kuvunja rekodi ya kuungwa mkono pamoja na kukifuta kivuli cha Besigye kwenye siasa za upinzani ikiwa na maana kwenda mbele zaidi kimafanikio kuliko kuishia alipoishia Besigye.

Nguvu kubwa ya ushindi wa Museveni imetajwa kutoka ufalme wa Buganda katikati ya taifa hilo.

Suala la kulinda na kuheshimu utawala wa kifalme wa Buganda ni miongoni mwa eneo muhimu la nguvu ya Museveni.

Upande wa kambi ya upinzani nguvu zao zilitegemea umoja wao, lakini uchaguzi wa mwaka 2021 mwanasiasa mwenye nguvu amejijenga binafsi ni Bob Wine huku akijikita na kundi la vijana ambalo limechagiza nguvu zake.

Duru za siasa zimebainisha kuwa mwanasiasa huyu anampa changamoto Museveni kuliko wakati wowote wa uchaguzi wa Uganda licha ya vikwazo anavyokumbana navyo.

Ni vipi vipaumbele vya Bobi Wine?

Kwa mujibu la hotuba aliyoitoa mjini Mbarara wakati wa kuzindua ilani, Bobi Wine alitaja vipaumbele; Kuboresha elimu,
Kufuta sheria kandamizi, Kulinda misingi ya demokrasia na diplomasia, Kuboresha afya, Wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni, Kutoa pedi bure, Kupambana na umasikini.

Pia, Kupambana na rushwa, Kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma, Kulipa mishahara ya walimu kwa wakati na kuwapa makazi, kuboresha maslahi ya madaktari,kuboresha mafunzo ya wafanyakazi na vifaa, Kujenga makazi watumishi wa vyombo vya dola,ajira milioni tano, Kuongeza uwekezaji katika teknolojia, kukusanya kodi, kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Ni upi mwelekeo wa Bobi Wine kisiasa? Mgombea huyo ana miaka 38 na huu ni uchaguzi wa kwanza nafasi ya urais.

Kwa umri huo anatengeneza kete muhimu kisiasa kwa miaka ijayo, ikizingatiwa anaungwa mkono na nguli wa siasa za upinzani Kizza Besigye.

Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa kama Bobi Wine hatoumizwa huenda akaja kuwa mpinzani mkubwa wa Jenerali Muhozi katika siasa miaka ijayo kwakuwa umri wake ni kete nzuri na anabeba ajenda ya vijana wa umri ule ambao haukushiriki mapigano japo baadhi wameonja utotoni sana kwa kukimbia na wazazi wao.

“Kwa namna Uganda, Bobi Wine akikomaa na Mungu akampa uhai anaweza kufaidika na siasa za mabadiliko zinazoweza kutokea miaka 30 mbele kutokea sasa ambazo hatujui zitakuwaje, japo kuna dalili kubwa kuwa zitakuwa ni za mrengo wa mashariki kwa maana ya China kwa kuwa ndiyo inayoonekana kuwa taifa lenye nguvu miaka ijayo.

Kwahiyo wanasiasa wanatakiwa kuelewa kesho ya nchi zao, wanapopigania mabadiliko namna hii kama Bob Wine, ni njia ya kuwakumbusha watawala, hawamiliki nchi, bali watapita na kuiacha,”

*Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mitandao

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here