BMT yampiga ‘stop’ miaka 2 Mwanjala kujihusisha na soka

0

NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Elias Mwanjala imeelezwa kuwa amefungiwa na Serikali kujihusisha na soka.

Mwanjala kupitia kamati hiyo iliamuru kuwa mkataba wa kiungo mshambuliaji raia wa Ghana, Bernard Morisson na Yanga ulikuwa na mapungufu kadhaa.

Ikumbukwe Yanga ilidaiwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili Morrison jambo ambalo alikana na kuwashtaki Yanga TFF kwa madai kuwa hakuwa ameongeza mkataba huo.

Hata hivyo siku chache kabla ya hukumu kutolewa, Morrison alitambulishwa kwenye kurasa za kijamii za Simba akisaini mkataba wa miaka miwili na mashabiki wa Yanga kuona kama Mwanjala alihusika kumpeleka mchezaji huyo kwa wapinzani wao, Simba.

Kwa mujibu wa Kaimu Msajili wa Vyama vya Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Malangwe Mchungahela, Mwanjala amevuliwa vyeo na nyadhifa zake zote katika michezo kwa kipindi cha miaka miwili.

Alisema kuwa kiongozi huyo ameondolewa nyadhifa hizo baada ya kupatikana na hatia ya kutwaa madaraka kinyume na utaratibu.

“Mwanjala amevuliwa vyeo na nyadhifa zake zote kwenye michezo na kufungiwa kujihususha na uongozi wowote wa michezo kwa miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kutwaa madaraka kinyume na utaratibu.

“Tayari Mwanjala amepewa barua kutoka Serikalini kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo nchini iliyokuwa chini ya Malangwe Mchungahela, ambapo kiongozi huyo amepewa adhabu hiyo kwa kukiuka Katiba ya Chama cha Soka cha Mbeya, ile ya TFF na FIFA.

“Na Serikali imeshawapa nakala ya uamuzi huo TFF kama waajiri wa Mwanjala,” alisema mtoa taarifa huyo.

Aidha, chanzo kingine kilisema “Yule aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya TFF iliyoamuru kuwa mkataba wa Morrison una upungufu na Simba kumchukua mazima amekutana na adhabu kubwa kutoka Serikali.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Watafutwe Chama cha Soka cha Mbeya wazungumzie, sisi hatujapata taarifa hiyo na kama tukiipata tutaitoa kupitia njia zetu rasmi za kutoa taarifa.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here