
NA SHAMIMU NYAKI – WHUSM, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa ametoa agizo kwa Bodi ya Filamu Tanzania kuhakikisha Kamati ya kusimamia Haki za Wasanii inafanya kazi hiyo kwa weledi na kasi kwa ajili ya maslahi ya wasanii.
Bashungwa alitoa agizo hilo juzi Desemba 15, 2020 alipotembelea Bodi ya Filamu Tanzania akiwa pamoja na Naibu wake Abdallah Ulega pamoja na Katibu Mkuu Dk. Hassan Abbasi ambapo ameitaka Kamati hiyo kuwasilisha serikalini Mpango mkakati wa namna inavyotekeleza jukumu hilo.
“Naiagiza Bodi ya Filamu nchini kuhakikisha maudhui na maadili ya filamu zinazotengezwa nchini zinakuwa bora ambazo zitaleta ushindani katika soko ndani na nje ya nchi, lakini pia lazima zizingatie utamaduni wa nchi yetu”,alisema Mhe.Bashungwa.
Aidha Waziri huyo aliongeza kuwa atahakikisha Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA zinakua katika jengo moja kwakua wadau wake ni wa aina moja, lengo ni kurahisisha huduma kwa wadau hao ambao wamekua na mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kuongeza ajira.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa wizara hiyo, Abdallah Ulega aliwapongeza wasanii wote nchini kwa kufanya kazi nzuri ambayo inawaingizia kipato na kuitangaza nchi vizuri pamoja na kukuza uchumi wa nchi, ambapo amesema mafanikio hayo yametokana na Sera nzuri ziliowekwa na Serikali kwa ajili ya kundi hilo, huku ankinukuu maneno ya Waziri Bashungwa kuwa “msanii kichwa chake ndio kiwanda chake”.
Ulega aliongeza kuwa Kamati inayosimamia Haki za Wasanii ifuatilie haki zote za wasanii ambao wameshatangulia mbele za haki kama marehemu Steven Kanumba na wengineo ili ziwanufaishe wanaohusika na marehemu hao.
“Nawaagiza Maafisa Utamaduni nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa kwakua ndio daraja la kuratibu na kusimamia kazi za sanaa kuanzia ngazi ya chini, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kazi za Sanaa na wasanii zinaratibiwa kwa kufuata mwongozo wa Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA pamoja na matwaka ya Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997”,alisema Ulega.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk. Hassan Abbasi alisema Taasisi hiyo imefanya mageuzi ya kiutendaji ikiwemo kuhuisha muundo kiutumishi kwakua ni taasisi mojawapo yenye dhamana madhubuti kwa wadau wake, huku aisisitiza kuwa Bodi hiyo itaendelea kufanya vizuri katika majukumu yake.
Hata hivyo Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dk. Kiango Kilonzo alisema mafanikio ambayo bodi imepata kuwa ni pamoja na kuonyesha filamu za kitanzania katika chaneli ya Maisha Magic Bongo ya DSTV, kusimamia chaguzi za vyama na mashirikisho ya filamu nchini, pamoja ni kupata Tuzo 200 za kitaifa kwa wadau wa filamu.