Barua za utambulisho wa mawakala wa uchaguzi kutolewa Jumanne

0

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi( NEC) Dk. Wilson Mahera amesema kuwa barua za utambulisho wa mawakala wa vyama vya siasa zitatolewa Oktoba 27 2020.

Mahera ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini hapa leo.

Akijibu swali aliloulizwa kuhusu malalamiko ya baadhi ya mawakala hao amesema sio jambo rahisi kwa wasimamizi kuwaapisha mawakala wote na kisha kuwapa barua za utambulisho hapo hapo.

“Bado wanaandaa barua za utambulisho za mawakala na zitapatikana tarehe 27. Ulikua ni mchakato mrefu na isingekua rahisi kutoa nyaraka hizo muda mfupi baada ya kuwaapisha,”amesema.

Aidha Mahera amesema tume imeweka utaratibu kwa wapiga kura ambao taarifa zao zitakuwa na makosa kwenye daftari la kudumu lakini wanavyo  vitambulisho vya kupigia kura.

Amesema watu hao wasiwe na hofu watapiga kura katika uchaguzi huo utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, 2020.

Pia amesema wapiga kura waliohama maeneo walioandikishia kupiga kura na hawajahamisha taarifa zao hawatapata nafasi ya kupiga kura za urais, ubunge wala udiwani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here