Amani yatawala Uchaguzi Mkuu

0

>> Magufuli awaongoza Watanzania kupiga kura kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani
>> Apanga foleni Kama wananchi wengine
>> Asisitiza kuna maisha na kuomba  amani iendelee kutawala

Na Hafidh Kido, Dodoma

AMANI, utulivu na mshikamano vimeendelea kutawala katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini Tanzania hii ikiwa ni ishara njema kwa maendeleo ya wananchi.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Magufuli jana alipiga kura katika kituo cha Idara ya Maji, Kijiji cha Ikulu Chamwino Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma ambapo aliwahimiza Watanzania kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Alibainisha, amevutiwa na hali ya utulivu na kila mmoja kutii sheria za nchi hasa suala la kurudi nyumbani au kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.

“Nawapongeza Watanzania kwa siku hii muhimu kwao katika kukuza demokrasia. Watu wamejitokeza kwa wingi, tunapiga kura kwa amani na utulivu naomba tuilinde amani yetu kwa kuwa ndicho kitu muhimu kwetu,” alisema Dk. Magufuli na kubainisha:

“Hakika kila mmoja anapopiga kura anakuwa ametimiza wajibu wake. Tujitahidi kuwa watulivu tusiwape nafasi watu wenye nia ya kuvuruga amani yetu.”

Aidha, Dk. Magufuli ambaye anaishi mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura cha Idara ya Maji ilipo Ikulu ya Chamwino, aliwasili kituoni saa 4:48 asubuhi akiwa ameambatana na mkewe Mama Janet Magufuli kisha moja kwa moja alipanga mstari ili kufuata utaratibu.

Wananchi walianza kujitokeza kuanzia saa 12 asubuhi kwa ajili ya kutimiza haki yao ya kikatiba, ambapo alipowasili Dk. Magufuli na mkewe walijumuika naye jirani yao kwenye foleni.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Dk. Magufuli kupiga kura, msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Chamwino yenye majimbo mawili
ya uchaguzi ya Chamwino na Mvumi, Athumani Masasi alisema Dk. Magufuli ameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kujumuika na wananchi wengine kwenye upigaji kura.

“Mgombea Dk. Magufuli amepiga kura kama mwananchi yeyote nchini, katika vituo vyetu tunao wasimamizi wasaidizi ili kila anayefika hapa panapotokea changamoto tunazitatua hapa hapa kituoni hakuna anayerudi kwa kukosa kupiga kura,” alisema Masasi na kueleza namna wanavyowasaidia watu wenye uhitaji maalum:

“Tumeweka utaratibu watu wenye mahitaki maalum tunawasaidia, hata wenye ulemavi wa macho kuna karatasi maalum.”

Siku ya jana ilikuwa ni alama ya kukamilisha miezi miwili ya kuzunguka nchi nzima kunadi sera za vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huu wa kidemokrasia.

Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika na pengine duniani ambapo kipindi cha uchaguzi wananchi wote wanakuwa wamoja na kuimarisha amani ili kuepuka machafuko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here