Almasi wenye thamani ya Bil.61 wataifishwa

0

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetaifisha mzigo wa madini ya almasi ambao ulikutwa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, ukiwa unasafirishwa kwenda nchini Ubelgiji, wenye thamani ya sh. bilioni 61, 970,625,864.

Almasi hizo zina uzito wa carats wa 71,654.45 ambazo zilikuwa zinasafirishwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania(TANSORT), Archard Kakugendo na Mthamini almas wa Serikali Edward Rweyemamu.

Pia mahakama hiyo, imewahukumu wathaminishaji hao ambao ni Kalugendo na Rweyemamu , kulipa faini ya sh. milioni moja kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuisababishia Serikali hasara sh. bilioni 61.9.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya, baada ya washitakiwa kuandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP), Desemba 17, mwaka huu ya kuonyesha nia ya kuingia makubaliano ya kukiri kosa lao.

Awali kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la mawakili watatu wa Serikali Wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Monica Mbogo, walidai shauri lilipelekwa kwa kutajwa na upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwa Mamlaka ya sheria ya Uhujumu uchumi, DPP ameridhika kuwashitaki washitakiwa katika mahakama hii.

Pia Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantore, alidai kesi hii ni Uhujumu Uchumi, hivyo DPP ameipa kibali mahakama hii kesi kusikilizwa.

Akiwasomea shitaka alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na shitaka la kuisababishia Serikali hasara ambapo alidai Agosti 25 na 31, mwaka 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa wa Dar es Salaam na Shinyanga, washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa wathamini wa Wizara ya Nisahati na madini walisababisha hasara ya dola za 29,509, 821.84, sawa na sh. bilioni 61.9

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here