Aina mpya ujangili wa tembo yabainika

0

NA JONAS MUSHI, DODOMA

BAADA ya mafanikio makubwa katika kupambana na ujangili ikiwemo ujangili wa tembo, imebainika uwepo wa mbinu mpya inayotumiwa na majangili.

Kutokana na kuimarishwa kwa njia za kupambana na ujangili wa tembo ikiwemo matumizi ya teknolojia na kuimarisha doria, majangili wamekuja na mbinu ya kuingiza imani potofu kwa wananchi ili washiriki katika mauaji ya tembo.

Akizungumza jana jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka na Wahariri wa Vyombo vya Habari, Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Dk. Allan Kijazi alisema katika siku za karibuni imeibuka imani potofu kwamba maini na mafuta ya tembo yanatibu saratani na vidonda vya tumbo.

Alisema baada ya uchunguzi walibaini ni mbinu inayotumiwa na majangili kujipatia meno ya tembo baada ya kuuliwa na wananchi.

“Hakuna ushahidi wowte wa kisayansi unaoonyesha maini na mafuta yanatibu saratani na vidonda vya tumbo kinachofanyika ni kutokana na kuongezeka kwa magonjwa hayo majangili wanatengeneza imani potofu  kwa lengo la kuwashawishi wanachi washiriki mauaji ya tembo na kisha wao hununua meno ya tembo,” alisema Dk. Kijazi.

Aliongeza kuwa wananchi wanatumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuweka sumu kwenye maboga na kuwategeshea misumari.

Aliwaonya watu wote wanaoshiriki katika aina hiyo ya ujangili kuwa watachukuliwa hatua bila kujali ni nani katika jamii.

Pia alisema kumekuwepo na ujangili wa biashara ya nyama ambazo huuzwa hadi nje ya nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa.

Dk. Kijazi alisema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria kwani upo utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha kila mwananchi anafaidi rasilimali za mali asili ikiwemo kupitia utalii na mabucha ya nyama pori yaliyoanzishwa hivi karibuni.

Alisema katika kipindi cha nyuma wananchi walikuwa wananwinda kwaajili ya kitoweo lakini hivi karibuni wamehamia kwenye kufanya biashara na kwamba watakao bainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here