ACT – Wazalendo yaridhia Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar

0

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kimeielekeza Kamati ya Uongozi ya chama hicho kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Pia imeazimia kuwaruhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wa chama hicho waliochaguliwa kwenda kukiwakilisha chama na wananchi waliowachagua.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Desemba 06, 2020 na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu wakati akitoa maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Akisoma maazimio hayo, Ado amesema; “Mosi kamati kuu ya chama chetu imeazimia wawakilishi wachache kwa maana ya madiwani, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge ambao wametangazwa kushinda waruhusiwe kushiriki kwenye vyombo vyao vya uwakilishi,” amesema Ado na kuongeza

“Pili Kamati Kuu ya chama chetu imeridhia chama kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi ya chama chetu kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,” amesema Ado akisoma maazimio ya kamati kuu ya chama hicho.

Amesema kuwa chama hicho kimefikia uamuzi huo kutokana na kupata mawazo ya kuwasikiliza wanachama na viongozi wa chama hicho.

“Kufikia uamuzi huu wa kuwaruhusu wanachama wetu kushiriki katika vyombo vya uwakilishi, tulijipa muda mrefu wa kutafakari, tulikwenda kuwasikiliza wananchi na wanachama wetu hasa kwenye maeneo waliopata madhila, pia tuliwashirikisha viongozi wa wetu wa ngazi zote.

“Tumefanya uamuzi huu, ili kuliponya Taifa, kurudisha mwangaza kwenye giza, kubwa zaidi tumefikia uamuzi huu kwa kuangalia maslahi makubwa ya Zanzibar na watu wake, maslahi ya chama chetu lakini pia maslahi ya Taifa kwa ujumla.” amesema Shaibu.

Aidha kuhusu kusambaa kwa taarifa kuwa aliyekuwa Mgombea Urais wa chama hicho   Benard Membe atajitoa katika chama hicho ifikapo Januari Mosi, 2021, amesema hawako  tayari kuzungumzia suala hilo kwa sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here