Mazao saba ya kimkakti anayopigania Majaliwa

0
Na Merciful Munuo, Kigoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amelitaja zao la Chikichi kuwa miongoni mwa mazao 7 ya kimkakati, ambayo serikali imewekeza nguvu zake katika kuinua na kuimarisha kilimo chake hapa nchini.

Waziri mkuu ameyasema hayo wakati wa mkutano na wadau wa sekta ya kilimo mkoani kigoma ambapo amesema kuwa kwa sasa nchi imeamua kuwekeza kwenye zao la Mchikichi, kutokana na uhitaji wa mafuta ya maweze ambayo nchi pia imekuwa ikiagiza nje ya nchi.

“Haiwezekani tuwe tuna mashamba ya kutosha, na yenye rutuba vizuri halafu tushindwe na majirani zetu ambao hawana ardhi kubwa kama ya kwetu” alisema Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Mkuu majaliwa aliyataja mazao mengine ya mkakati kuwa ni pamoja na Tumbaku, Chai, Kahawa, Pamba, Katani (Mkonge), zao la Chikichi pamoja na Korosho.

Vilevile Majaliwa pia amezitaka taasisi za kibenki kutoa mikopo yenye riba nafuu na kuhakikisha kuwa wakati wa kurejesha mikopo hiyo unaendanana na wakati wa kuvuna kwa mikopo ya wakulima ili kutowakwamisha kwenye urudishaji wa madeni yao ili waweze kuwekeza kwenye mazao ya kimkakati ikiwemo zao la chikichi.

“Hili suala la mikopo muangalie muwe na vifurushi vya walau miaka mitatu kwa wakulima hawa maana hauwezi kumpa mkulima kifurushi cha miezi sita halafu yeye anategemea kuvuna baada ya miaka mitatu utamdai tu” alieleza Majaliwa

Katika hatua nyingine Majaliwa alieleza kuwa mazao haya ya kimkakati, ikiwa yatapewa kipaumbele yatasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja pamoja na nchi kwa ujumla kwani uhitaji wa mazao haya ni mkubwa duniani.Vilevile Majaliwa pia amemuagiza Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda kutafuta wawekezaji wa kilimo cha zao la chikichi pamoja na kutoa mashamba kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo cha zao hilo.

Wakati akijibu maswali ya wadau wa sekta hiyo wakiwemo wakulima walikuwa wakijadili hoja mbalimbali, pia ameagiza tafiti kufanyika ili kubaini ikiwa kuna ugonjwa umeingilia zao hilo pamoja na kutafuta maeneo yenye ardhi yenye rutuba kwaajili ya kilimo chake.

Zao la chikichi limekuwa miongoni mwa mazao muhimu duniani, kutokana na uzalishaji wa mafuta ya mawese ambayo yamekuwa yakitumika kama mafuta ya kupikia pamoja na tiba.

Kwa mujibu wa rekodi za mtandao wa wikipedia nchi zinazoongoza zaidi kwa kilimo cha michikichi ni pamoja na nchi za Malaysia na Indonesia zenye mavuno ya asilimia 80 ya mawese duniani, huku nchi za Brazil na Kolumbia zikiwa zimeanza kupanda Michikichi kwa wingi.

Uthai, Papua–guinea mpya na nchi za Afrika ya magharibi zinachangia asilimia ndogo kwenye soko la dunia ya michikichi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here