Rais Magufuli: Chapeni Kazi

0

NA DOTTO KWILASA, DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dk.John Magufuli amesema kuwa Katika Serikali yake hana mpango wa kubadilisha wakuu wa mikoa,wilaya,wakurugenzi wa halmashauri,makatibu wakuu waliopo na kuwataka kuendelea kuchapa kazi.

Dk.Magufuli alitoa kauli hiyo jana  Ikulu Chamwino jijini Dodoma wakati akimuapisha mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, ambapo alisema kuwa mabadiliko yatatokea endapo utendaji wa kiongozi husika utakuwa hauridhishi au amestaafu au aamue kujiuzulu.

Alisema kuwa ameamua kuzungumzia suala hilo ili kuwaondoa hofu watendaji ambao  baadhi yao wameanza kumtumia ujumbe kuashiria hofu ya kustaafishwa na kusisitiza kuwa  alianza nao na atamaliza nao.

Rais Magufuli alisema  utendaji mzuri wa watumishi hao umechangia chama cha CCM kupata ushindi wa asilimia 84.4 kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwani kazi ya kuapisha inachosha na kuwa hawezi kuifanya kila akiingia madarakani.

 “Kwa sasa hivi wana hofu sana wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na ninawashangaa kwa nini wanakuwa na hofu kwa sababu kama ni mafanikio ya Serikali ni pamoja na wao,” alisema.

“Mkuu wa mkoa unakuwa na wasiwasi gani, labda kama utendaji wako haukuwa vizuri, kwa sababu nashangaa napata vimeseji vingine, ‘mheshimiwa, Rais nimejitahidi katika kipindi changu’ kana kwamba nilimwambia kipindi chake kinaisha baada ya mimi kuapishwa,” alisema Rais Magufuli .

“Nimeona hili nilizungumze kwamba wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya msiwe na wasiwasi na inawezekana wala pasitokee badiliko hata moja labda kwa mtu atakayestaafu au atakayefanya mambo ya hovyo sana.

“Kwa nini nibadilishe mkuu wa mkoa,” aliongeza.

“Najua inawezekana wananisikia, wachape kazi, wasipochapa kazi shauri yao, labda waandike barua ya kuondoka lakini najua nilianza nao. Wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya, Wakurugenzi, makatibu tawala na wengine katika maeneo mbalimbali wachape kazi hakuna cha kuwa na wasiwasi. Kama nilikuteua mwaka jana au miaka miwili iliyopita si uwezo ule ule na mtu ni yule yule kama wananisikia nawaambia wachape kazi nitaanza nao na nitamaliza nao. Natoa wito kwa watendaji wa Serikali wachape kazi katika nafasi zao kwa maana nyingine hakuna mabadiliko, tulianza wote tutamaliza wote,” alisisitiza.

Alieleza kuwa eneo ambalo atafanya mabadiliko ni kwa mawaziri.

 “Mabadiliko yatakayokuwepo ni kwenye mawaziri, kuna ambao watarudi na kuna ambao hawatarudi hili sitaki kusema uongo, nikishamaliza hilo basi wengine wachape kazi tu,” alisema Rais Magufuli.

”Mabadiliko yatakuwepo ni kwenye nafasi tu zile za uwaziri ambazo zenyewe tulienda kuomba upya.Wapo watakaorudi wapo ambao watarudi ,tena siku hizi option (machaguo) ni kubwa,nina wabunge 264, kwa hiyo uchaguzi ni mkubwa zaidi,” alisema Rais Magufuli.”

Akizungumzia kuhusu kumteua tena Profesa Kilangi kuwa AG alisem ani kutokana na utendaji wake mzuri katika awamu iliyopita na kwamba naamini atafanya vizuri zaidi katika awamu hii.

“Nakuagiza ukaisimamie vizuri ofisi yako ili yale yanayohusu maslahi makubwa katika ofisi yako ukayashughulikie kweli kwani kazi hii ni dhamana basi tupo kwa niaba ya Watanzania katika kipindi chako umejitahidi umefanyakazi vizuri na ndio maana nimekupa tena ukaifanye kazi hiyo vzuri zaidi,” alisema.

“Majukumu makubwa ulio nayo kila mahali upo na nafikiri utatusaidia zaidi na mimi nakupongeza sana lakini kikubwa ukamtangulize mungu katika jukumu lako kwasababu ni jukumu kubwa. Watanzania wangependa kuona mafanikioo makubwa na wasingependa kuona kesi za serikali zinashindwa wakati Mwanasheria ni mzuri ana professional, na uzoefu mkubwa.

“Watanzania wangependa kuona kesi zao zinatatuliwa mapema aliyekupa pole na mimi nakupa pia kwasababu unatakiwa kwenda kufanya kazi kwelikweli.

“Katika kipindi chako cha mwanzo ulifanya kazi vizuri ndio maana tumekupa tena ukaifanye vizuri zaidi kikubwa ukamtangulize Mungu mbele,” alisema Rais Magufuli.

Awali akizungumza mara baada ya kuapishwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof.Adelardus Kilangi alimshukuru Rais kwakuendelea kumuamini na kumpa nafasi hiyo kwa mara ya pili na kuahidi kufanya kazi kwa bidii katika kumsaidia Rais.

 “Ninaanza majukumu haya nikiwa naanza kipindi hiki cha pili nikiwa na uelewa zaidi juu ya majukumu ya serikali lakini pia naahidi kukabiliana na changamoto zozote  kwa namna moja katika utendaji wangu,”alisema

Kwa upande wake Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuteuliwa tena katika nafasi hiyo kwa mara nyingine akiamini kuwa imani huzaa imani ndio maana Rais Magufuli kamteua tena na ana matumaini ataendelea kufanya kazi kwa bidii.

 Aidha alisema kuwa kwa nafasi aliyonayo Mwanasheria Mkuu huyo anazunguka kote ndani ya serikali hivyo atampa ushirikiano pale itakapohitajika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here